28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

‘DIMBA MUSIC CONCERT’ LIMEONYESHA UHITAJI WA DANSI NCHINI

NA VALERY KIYUNGU

WAKATI mwingine tena tunakutana katika safu hii ya Old Skul, inayokukutanisha na wanamuziki wa muziki wa dansi, wakongwe ambao waliwahi kufanya vizuri katika tasnia hiyo miaka mingi iliyopita.

Siyo jambo baya leo Old Skul tukilizungumzia tamasha la Dimba Music Concert, ambalo lilifanyika Septemba 2, mwaka huu, kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam, lililoikutanisha bendi kongwe ya Msondo Ngoma, dhidi ya mastaa wa muziki kikosi cha timu ya Taifa ya Dansi.

Onesho hilo kwa kiasi kikubwa limeweza kukusanya mashabiki wengi wa muziki wa dansi, ambao walitoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na vitongoji vyake, nadiriki kusema kuwa, baadhi yao walisafiri kutoka mikoa ya jirani.

Dimba Music Concert limedhihirishia mashabiki uwepo wa muziki wa zamani wa dansi hapa nchini, tofauti na dhana iliyojengeka kwa watu ambao hawautakii mema muziki huo kuwa umetoweka au unaelekea kufa.

Siku ile nilikuwa miongoni mwa waliofika ukumbini kushuhudia tamasha lile, naamini kwa wengine ambao nao pia walihudhuria mtanange ule watakubaliana na mimi kuwa muziki wa dansi wa zamani ungalipo, pia una nafasi yake hapa nchini.

Ni muziki wa zamani ndio uliowarudisha nyuma mashabiki ukumbini pale, kiasi baadhi yao walifikia hatua ya kutoa machozi ya furaha, kutokana na baadhi ya nyimbo zilizotumbuizwa kutochuja, licha ya ukweli kwamba zilitungwa na kupigwa katika miaka ya 1979 na 1980.

Wakizungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baadhi ya washiriki wa onyesho hilo wanasema kuwa, muziki wa zamani bado upo, kwa maelezo kuwa wanamuziki wa muziki huo wangali wapo na wanaendelea kufanya vizuri kwenye bendi walizojiunga nazo.

Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ anasema kuwa yeye na washiriki wenzake kwenye onyesho lile, waliweza kuwaonyesha mashabiki jinsi muziki wa zamani unavyopigwa, kadhalika namna unavyoenziwa na walengwa, licha ya sasa kuwa na ‘umri mkubwa’.

“Kwa kuwa sisi ambao tulipiga muziki zamani tupo, ikubalike kuwa muziki huo pia upo na  unaendelezwa, ombi langu ni kwamba tupewe nafasi ya kufanya maonyesho mengi zaidi ya aina hii,” anasema mkongwe huyo, ambaye pia aliomba yawe yanafanyika mikoani.

Juma Katundu, mwanamuziki wa bendi kongwe ya muziki wa dansi, anasema kuwa ameungana na wakongwe kuendeleza muziki wa zamani, kwani licha ya yeye kuwa chipukizi katika tasnia hiyo, anashirikiana na wanamuziki wa zamani kwenye bendi ya Msondo Ngoma.

Hussein Jumbe, ambaye ni kiongozi wa bendi ya The Talent, anasema kuwa, tamasha la Dimba Music Concert limeondoa kabisa dhana potofu kutoka kwa baadhi ya mashabiki, juu ya kutoweka kwa muziki wa zamani masikioni mwa mashabiki.

Tamasha lile ni la pili kufanyika hapa nchini, likihusisha wanamuziki wakongwe. Tamasha la kwanza lilifanyika mwaka 1986, likijulikana kama Tanzania All Stars, ambalo lilishirikisha wanamuziki nyota 56.

Baadhi ya wanamuziki waliounda kundi hilo ambalo lilifanya kazi nzuri ni Marijani Rajabu, Maalim Gurumo, Nana Njige na Zacharia Daniel, ambao walitunga nyimbo na kuimba kwa kutumia lugha tano ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kireno, Kihindi na Kifaransa.

Usikose kuangalia yaliyojiri kwenye Dimba Music Concert leo saa 12 jioni kupitia runinga ya TBC One na kesho Jumapili saa 10 jioni, hali kadhalika Jumatano saa 9 alasiri.

Maoni yako yalete hapa 0714288656

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles