NA BEATRICE KAIZA,
BAADA ya miaka miwili kupita bila kufanyika kwa shindano la Miss Tanzania na taji kumilikiwa na mrembo Lilian Kamazima, juzi shindano hilo lilifanyika jijini Mwanza kwa mara ya kwanza na mrembo kutoka Kinondoni, Dar es Salaam, Diana Edward, ameibuka mshindi wa taji hilo kati ya warembo 30.
Katika mashindano ya mwaka huu kama kawaida ya mashindano hayo, walimbwende walipanda jukwaani na kuonyesha uwezo wao wa kutembea na kujibu maswali yaliyoandaliwa na majaji.
Baada ya mchakato wote kukamilika, mrembo Diana alitangazwa kuwa mshindi wa shindano hilo kwa mwaka 2016, huku nafasi ya pili ikishikwa na Maria Peter na mshindi wa tatu akiwa ni Grace Malikita.
Mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, alimkabidhi zawadi ya gari mshindi wa kwanza, Diana Edward mara baada ya kutangaza kuwa mshindi.
Mrembo huyo ataiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya dunia yatakayofanyika Desemba 8 mwaka huu, huko nchini Marekani.