22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

DIAMOND CHEZEA FEDHA USICHEZEE NAFASI ULIYOPO

NA MWANDISHI WETU

MTAJI mkubwa wa msanii yeyote yule kwenye tasnia ya muziki ni mashabiki. Kila siku mwanamuziki hutafakari jambo gani afanye ili aongeze idadi ya wafuasi na hapo ndipo tunaona wasanii wakishindana kufanya kazi nzuri zinazowaweka kwenye chati.

Hakuna ubishi Diamond Platnumz ndiye msanii mwenye mashabiki wengi kwa sasa. Ana mtaji mkubwa wa watu ambao wamekuwa wakimpa sapoti kila anapofanya sanaa yake, hajawahi kuwaangusha, ndiyo maana wameendelea kumuaminia.

Lakini inakuwaje pale nyota wa Bongo Fleva kama yeye anapoamua kuchezea nafasi aliyonayo kwa kuwagawa mashabiki ambao kwake ni muhimu kuliko kitu chochote anachojihusisha nacho, mfano siasa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Diamond Platnumz aliibuka na wimbo alioupa jina la Acha Nikae Kimya. Ni wimbo wa ghafla uliokusanya visa, mikasa na matukio yaliyotokea kwenye jamii yetu siku za hivi karibuni.

Wimbo huo una melodi nzuri, ila ujumbe, hasa uelekeo wake ulionekana wazi kuwagawa mashabiki zake, ndiyo maana haukupata mapokezi makubwa kama nyimbo zake za nyuma.

Kabla ya kutoa wimbo huo wa ghafla, Diamond alikuwa anatamba na singo ya Marry You, aliyomshirikisha msanii wa Marekani, Ne-Yo. Ni wimbo mzuri ambao mpaka sasa kwenye mtandao wa YouTube umetazamwa mara milioni 8.4.

Sasa kutoka kwenye kiwanga cha juu cha wimbo wa Marry You mpaka kuja kuibuka na wimbo uliopingwa karibia na nusu ya mashabiki wake ni hatari mno kwa ustawi wa muziki wake, hasa ile nafasi aliyonayo ambayo wasanii wengi wanaitamani.

Sikatai msanii kuimba matatizo ya jamii yake, lakini inategemea na ujumbe umelenga nini hasa kwenye jamii yako. Tumesikia Wapo, wimbo ulioimbwa na msanii Nay wa Mitego unagusa moja kwa moja maisha ya watu, ndiyo maana raia, mpaka Rais Dk John Magufuli ameupenda.

Diamond ni mfanyabiashara, ametambua alichokifanya, ndiyo maana amekuwa mpole na kupunguza nguvu ya kuusukuma wimbo huo, sidhani kama hata video ya Acha Nikae Kimya ataifanya.

Si hivyo tu, amejisafisha mbele ya mashabiki kwa kuweka picha kwenye mtandao wake wa Instagram unaomwonyesha yupo na staa wa RnB Afrika Kusini, Donald, kuashiria kuna kazi mpya inakuja, halikadhalika kuweka picha ya Chris Brown ili watu walioanza kumchukia warudi kwenye mstari wa kusapoti kazi zake kama zamani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles