Anna Potinus, Dar es Salaam
Kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi imemtambulisha rasmi msanii wa muziki kizazi kipya (Bongo Fleva), Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz kuwa balozi wa kinywaji hicho.
Utambulisho huo ulifanyika jana jijini Dar es salaam ambapo Diamond ameahidi kuwa balozi bora wa kinywaji hicho na kuhakikisha vijana wote wanakitumia.
Diamond alisema anafurahi ‘shavu’ kutoka kwa kampuni kubwa kama Pepsi kwani sasa anaingia familia moja na wasanii wakubwa kama vile Tecno wa Nigeria, msakata Kabumbu wa Barcelona, Lionel Messi, Beyonce na wengine wengi wanaotangaza bidhaa za Pepsi duniani.
“Kupata shavu kama hili kwangu mimi ni hatua kubwa kwani unaweza kuwa balozi wa tu ilimradi upate fedha, lakini Pepsi ina watu wenye heshima duniani kwa hiyo mimi sasa hivi ni kama kina Michael Jackson hivi na juzi tu nimemsikia dada yangu Cardi B, akitangaza Pepsi.
“Pepsi ni watu ambao wamekuwa wanathamini vipaji vya vijana pamoja na vijana wao na hii kwangu ni fursa kubwa na ninatakiwa niitendee haki kwani kwa kufanya hivyo kutatengeneza mianya kwa wasanii wengine kuwa mabalozi katika vitu tofauti.
“Mimi ni mpenzi wa bidhaa za Pepsi na zamani kabla sijaanza kufanya nao kazi nilikuwa nazitumia huku ninajificha lakini sasa hivi niko huru kutembea nazo popote lakini pia ni kitu ambacho ninakipenda ndiyo maana ninaamini nitakuwa balozi mzuri,” amesema Diamond.
Kwa upande wake Meneja Mafunzo na Uwezeshaji, Rashid Chenja, amesema wamefikia uamuzi wa kumchagua Diamond kuwa balozi kutokana na uwezo wake wa kutoa burudani za kipekee.
“Tulivyokuwa tunafikia maamuzi ya kuzindua ‘Mkubwa Wao’ tulijua kwamba ilikuwa muhimu sana tushirikiane na mtu maarufu, mtu huyo ilikuwa ni lazima awe mtu anayetuletea burudani na yeye, na kwa umaarufu wake aweze kujulikana kama ‘Mkubwa Wao’ kama yeye.
“Na tulivyoona jinsi mwimbaji huyu alivyojitahidi kujipatia umaarufu nchini na kimataifa na jinsi anavyoendelea kutengeneza miziki inayotuburudisha kila inaposikika, tulijua kwamba balozi wetu wa Pepsi Tanzania mwaka 2019 lazima awe mkubwa wao mwenyewe Diamond Platinumz,” alisema.