Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa azma ya Serikali ni kuimarisha na kuongeza uwezo kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili iweze kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kulea vizuri vijana.
Kauli hiyo imetolewa leo na Rais Dk. Samia wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri uliopo jijini Dodoma.
“Dhamira ya Serikali ni kuimarisha JKT ili liwe Jeshi la kisasa zaidi linaloendana na wakati na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu, mafunzo yanayotolewa na JKT yawasaidie vijana kuwa wazalendo wa kweli wanaothamini utaifa, umoja na mshikamano wa Watanzania na wanaopenda kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea,” amesema Dk. Samia.
Aidha, katika hatua nyingine Rais Dk. Samia alisisitiza: “Naelekeza Wizara ya Ulinzi na JKT kuandaa mpango mkakati wa kurekebisha makambi kwenye Jeshi la JKT katika upande wa malezi ya vijana. Aidha, kuliwezesha Shirika la SUMA JKT kupata mikopo ili wazalishe na waweze kurejesha mikopo na shirika liweze kuendelea, na kama ikitakiwa udhamini wa Serikali, tuko tayari kuwezesha SUMA- JKT ili iweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda alisema kuwa JKT inatekeleza shughuli za uzalishaji mali na ulinzi wa taifa, pia inaendelea kutekeleza majukumu yake mengine ya msingi na kuhakikisha kuwa mawazo ya Hayati Mwl. Julius Nyerere katika uanzishwaji wake yanadumishwa kwa vitendo.
“Naishukuru Serikali kwa kuendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo kwa kulipatia Jeshi hili rasilimali mbalimbali kwa nia ya kuliwezesha Jeshi kutimiza malengo yake kwa ufanisi zaidi. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na JKT, tumeweka mikakati ya kuliboresha na kulifanya Jeshi la Kujenga Taifa kuwa la kisasa zaidi ili liweze kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani”, alieleza Mkuu wa Majeshi.
Naye, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele alisema kuwa, dhumuni kuu la kuadhimisha miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa tangu kuasisiwa kwake ikiwa na lengo la kutoa mafunzo ya malezi kwa vijana, kuwajengea uzalendo, uadilifu, uvumilivu, mshikamano na kupenda kazi hatimaye kuwa na vijana wanaoweza kujitegemea na kuwa tayari kuitumikia na kuilinda nchi ya Tanzania.
Meja Jenerali Mabele alifafanua kuwa, JKT imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kubadilisha fikra za kikoloni kwa vijana waliohudhuria mafunzo yake, kuwajenga vijana katika hali ya umoja, moyo wa kupenda kazi, uadilifu, nidhamu, uelewano bila kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini, jinsia hivyo kudumisha uhuru na amani ya Taifa.
“JKT imefanikiwa kuwa na ongezeko la idadi ya vijana wanaopata mafunzo ya Jeshi hili ambapo mwanzo lilianza na vijana 11 lakini kwa sasa vijana waliopo makambini wanaohudhuria mafunzo kwa mujibu wa Sheria ni 52,000,” alimaliza Meja Jenerali Mabele.
JKT ilianzishwa rasmi Julai 10, 1963, hatua hii ilikuwa ni utekelezaji wa azimio la kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Aprili 19, 1963 chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwl. Julius Nyerere.