SIJAKOSEA kumvika kilemba cha Unabii Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere si tu kwa kusadifu sifa hiyo, bali pia maana halisi ya asili ya sifa hiyo kwani Nabii ni binadamu anayesema kwa niaba ya Mungu akiwaelekeza wenzake kufuata imani.
Nabii imetoholewa kutoka Kigiriki (Prophētēs) hadi Kiingereza (Prophet) yaani anayesema jambo hadharani kabla halijatokea kwa muktadha wa imani, lakini maana ya pili ni mtu anayetabiri jambo kutokana na karama ya kulitambua kabla halijajiri bila kujali amelifahamu kwa njia gani, hapo ndipo Mwalimu Nyerere anapojipatia sifa hiyo kutokana na hotuba zake nyingi kubainisha matukio ya kisiasa yatakayotokea siku za usoni hapa nchini na hata kimataifa kutokana na kauli zake.
Nikinukuu moja ya hotuba zake aliwahi kutanabaisha: “Dhambi ya ubaguzi ukishaitenda utaendelea tu kuitenda, ni sawa na kula nyama ya mtu ukishaila utaendelea tu kuila!” mwisho wa kunukuu. Ndicho kinachoyakumba mataifa makubwa kwa sasa hususani ya Magharibi maana dhambi waliyoitenda ya kubagua maslahi ya wengine sasa inaendelea kuwatafuna kwa kubaguana wenyewe kwa mambo yaliyoonekana mepesi kukubaliana baada ya mchakato wa kuyatimiza uliochukua siku nyingi.
Rais Donald Trump wa Marekani alimaliza ziara yake ya hivi karibuni ya mataifa mbalimbali kwa kukorogana na viongozi wenzake wa G-7 na kusababisha mkanganyiko, katika muktadha wake wa ‘Marekani Kwanza’ alipowakatalia kuidhinisha mkataba wa upunguzaji wa hewa ya ukaa baada ya kikao kilichogubikwa na mabishano makali, wakaishia kukanganyikiwa kutokana na malumbano makali kwani ilidhaniwa kuwa mchakato huo ulioridhiwa miaka miwili iliyopita umeshakamilika, hali iliyosababisha misimamo ya mataifa mengine kuyumbishwa akiwamo Rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Katika mvutano huo kwenye kikao kilichofanyika Taormina, Sicily nchini Italia Trump alijitenga kimsimamo ingawa ndani ya uongozi wake pia kuna fukuto la mkanganyiko kutokana na kusigana, Trump akishikilia kuwa kukubaliana na mkataba wa Paris ni kusababisha kupotea kwa ajira lukuki kwa Wamarekani lakini kuna wanaopingana naye ambao wanataka Marekani iwe mshirika mkubwa wa kudhibiti uchafuzi wa hewa duniani, kwani unaathiri si tu mazingira lakini pia maisha ya viumbe mbalimbali wakiwamo wanadamu.
Ni kizungumkuti kingine kinachomkabili Trump ambaye hajamaliza sekeseke la tuhuma za kudukuliwa kwa hiari na Urusi linalorindima Marekani linalosababisha wasaidizi wake waandamizi kujiuzulu, lakini pia ameziba masikio hasikii la mnadi swala wala la muadhini kwani alimpuuza hata Papa Francis kwa wito wa maridhiano na kusababisha Marekani ijitenge na nchi nyingine 195 zilizosaini makubaliano hayo.
Lakini pia ametia chachandu kwenye kidonda alipokoromea sera za kibiashara za Ujerumani na kuwashutumu wanachama wenzake wa NATO kwa kutowekeza juhudi za kutosha katika kuimarisha Umoja huo wa Kujihami wa Nchi za Magharibi.
Ziara yake ambayo wengi wanaiona kama aliitumia zaidi kukimbia ‘vimeo’ vinavyomkabili nyumbani inakanganya kwani wakati akiwa nje, mkwewe, Jared Kushner, ambaye ni mmoja wa washauri wake alimwaga mtama kwenye kuku kwa kudhihirisha mawasiliano ya siri na Urusi kabla Trump hajasimikwa rasmi madarakani. Licha ya kujidhibiti alipokuwa Israel na Saudi Arabia amewakasirisha Ulaya kwa kukataa kipengele cha tano cha mkataba wa NATO kinachoilazimisha Marekani kuingilia kati kijeshi mmojawapo wa wanachama anaposhambuliwa, lakini pia akiwa mwingi wa hasira alimpiga kumbo Waziri Mkuu wa Montenegro wakati wa kupiga picha kama mwanamieleka anayejiandaa kumbidua mpinzani wake licha ya washauri wake kumsihi kuwazingatia washirika wa Marekani lakini hakuwasikiliza.
Baada ya kurudi Trump ametoa kauli kwamba anasitisha ushiriki wa Marekani katika mkataba huo hadi yapatikane makubaliano ambayo hayataathiri ajira za Wamarekani, lakini hatua hiyo imesababisha mkanganyiko mkubwa kwa kusigana na washirika wa Ulaya wanaomtuhumu kwa kupika takwimu zilizokosa ithibati kwa kushikilia uhafidhina wa ‘Marekani Kwanza’ kwa madai kuwa ajira milioni 2.7 zitapotea ikiwa wataendelea na makubaliano hayo, ingawa ukweli ni kwamba angeridhia ingesaidia kupunguza majanga ya asili kwenye ukanda wa bahari nchini mwake yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanayochagizwa na wingi wa gesi za sumu kutokana na viwanda.
Fukuto hilo limesababisha athari kadhaa, mojawapo Ulaya kutafuta mshirika wa kushikamana naye kutokana na Marekani kuwapa kisogo wakaigeukia China ambayo nayo imewachomolea kutokana na kisingizio cha mbinyo wa kibiashara iliyofanyiwa kwenye WTO, ingawa kwa uhalisia hata nayo ikiridhia itakuwa inaua viwanda vyake wakati inahitaji kuikaba koo Marekani ili kuipiku kiuzalishaji.
Ufaransa na Ujerumani walau zinazungumza kauli zinazorandana lakini Uingereza ni kama inashabikia kisirisiri hatua ya Marekani, kutokana na hatua yake ya kujitoa EU kutofurahiwa na washirika wenzake ndipo usemi wa Hayati Mwalimu Nyerere unapotimia kwani ubaguzi wa kutojali maslahi ya dunia kwa ulafi wa uchumi wa kushindana kiviwanda unaosababisha kuchafua hewa ya dunia, sasa unayatafuna mataifa hayo makubwa yanayosigana na kushindwa kuelewana ingawa kwa uhakika mvutano wao unaumiza wengi kwani athari za mabadiliko ya tabia nchi ziko wazi hata barani Afrika, ikiwamo kubadilika kwa majira na misimu na kusababisha mvua zisizo na ukomo zilizorefusha muda wa kunyesha.