32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Dhamana ya kina Kitilya yanukia

Harry KitilyaNA MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana imetupilia mbali rufaa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP), dhidi ya Kamishna Mkuu wa zamani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mosses Mzuna, alisema uamuzi huo umetokana na hoja zilizowasilishwa na mawakili wa pande zote mbili ambao hauwezi kusikiliza rufaa hiyo.

“Rufaa ya DPP haina miguu, nimeamua kuiondoa nendeni mahakama ya chini hivyo nimeamua kutupilia mbali, lakini nimetoa nafasi kwa upande wa Jamhuri kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka namba nane linalowakabili washtakiwa.
“Kufutwa kwa shtaka hilo sio kwamba shauri limemalizika kwa kuwa hali hii itakuwa ni sawa na kuwanyima haki ya kuendelea na shauri hilo, kwa sababu kila kesi inaamuliwa kulingana na mazingira yake,” alisema Jaji Mzuna.

Pia alisema sababu mojawapo iliyofanya mahakama hiyo kutoa uamuzi huo ni kutokujua kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitoa nafasi kwa upande wa Jamhuri kubadili shtaka namba nane ama la.

Kwa upande wa Jamhuri uliokuwa ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis, ulidai kuwa wao wanakubaliana na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo ila bado hawajaafikiana hivyo watakaa na kujadiliana ili kubadili hati hiyo ya mashtaka.

“Kwa sasa siwezi kusema kitu cha msingi ila bado tuna uwezo wa kupeleka maombi yetu baada ya kupewa huo uamuzi uliotolewa hapa tutakaa tuusome tuangalie namna ya kubadili shtaka hilo,” alisema Wakili Vitalis.

Kwa upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na Wakili Majura Magafu, Dk. Ringo Tenga na Alex Mgongolwa, walidai kwamba wao wanasubiri watakachokifanya Jamhuri endapo wakibadili hati hiyo.

“Hapa tayari sheria imeshachukua mkondo wake hivyo kilichobakia ni kufuata maelekezo, Jaji Mfawidhi inabidi shauri lirudi Kisutu kwa ajili ya kuendelea, tunawasubiria walete maombi yao aidha yawe ya maandishi au maongezi sisi tutajibu,” alidai Magafu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Miss Tanzania (1996), Shose Sinare na Mwanasheria wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Sioi Solomon.

Washtakiwa hao pamoja na mashtaka mengine, wanadaiwa kutakatisha dola milioni sita za Marekani kwa kuzihamisha kutoka katika akaunti ya Kampuni ya Egma.

Hata hivyo, Aprili 27, mwaka huu, Mahakama ya Kisutu iliwafutia shtaka hilo na kubakiwa na mengine ambayo yanadhaminika baada ya upande wa utetezi kuiomba mahakama iliondoe kwa madai kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria kwa kuwa hakuna maelezo ya wazi jinsi walivyotenda kosa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles