Na Kulwa Mzee, Dar es SalaamÂ
Kigogo wa IPTL, James Rugemarila amewasilisha maombi Mahakama ya Rufani akiomba apewe dhamana na  kufanya marekebisho katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa kunyimwa dhamana na Mahakama Kuu.
Rugemarila anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu amewasilisha maombi hayo leo Jumatatu Machi 5, mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Bernard Luanda, Batuel Mmilla na Gerald Ndika.
Pia anaiomba mahakama hiyo aweze kumuweka Harbinder Sethi kama mtu muhimu na impatie dhamana wakati rufani yake ikiendelea kusikilizwa.
Sethi ambaye alikuwapo mahakamani ambapo mawakili Pascal Kamala na Magdalena Rwebangira walijitambulisha kumwakilisha Rugemarila ambapo baada ya Rugemarila kuwasilisha maombi hayo, Februari 28, mwaka huu, upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo.
Akiwasilisha hoja za pingamizi la awali, Mawakili wa Serikali wakuu, Dk. Zainabu Mango, Peter Maugo na Tumaini Kweka walidai maombi hayo hayapo sahihi mahakamani hapo kwa kuwa yamewasilishwa kwa kanuni zisizo sahihi.
Dk. Zainabu alidai mleta maombi amewasilisha maombi hayo kwa kutumia kanuni mbalimbali za Mahakama ya Rufani, hivyo kuyafanya yashindwe kueleweka kama ni ya madai, jinai au anaomba marejeo.
Awali Rugemarila na Sethi waliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, ambayo yalitupiliwa mbali. Kutokana na hilo, Rugemarila aliwasilisha Mahakama ya Rufani taarifa ya kusudio ya kukata rufani kupinga uamuzi huo.
Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ambayo ina mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.