Na Hassan Daudi, Dar es Salaam
Ama hakika unaweza kusema ni zaidi ya burudani kwa mashabiki wa kandanda la Bongo, hasa wanazi wa klabu kongwe hizi za Simba na Yanga.
Ni ‘derby’ ya Kariakoo na safari hii, kwa maana ya kesho (Mei 8, 2021), wenyeji Simba watashuka dimbani wakiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya Yanga.
Wekundu wa Msimbazi wamejikusanyia pointi 57 wakiwa wamecheza mechi 25, wakati Yanga wanashika nafasi ya pili wakiwa wana pointi 53 kwa michezo yao 27.
Uko wapi ugumu wa mechi hii?
Ukizungumzia umuhimu wa mechi hii unaweza kuugawa katika maeneo mawili. Mosi, kama inavyofahamika, matokeo ya ‘derby’ huwa na umuhimu mkubwa kwa mashabiki wa Simba na Yanga, bila kujali pointi tatu zitakuwa na faida gani katika ‘ishu’ ya ubingwa.
Wakati mwingine, saikolojia ya mashabiki wa klabu hizi itakwambia pointi tatu za ‘dervy’ ni muhimu zaidi kwao kuliko sherehe za kulitwaa taji la Ligi Kuu Bara.
Pili, endapo Simba watashinda, basi watakuwa wameiacha Yanga pointi saba, wakati huo pia ikiendelea kubaki na mechi mbili mkononi.
Ukweli ni kwamba Yanga hawatakuwa tayari kuona hilo likitokea, hasa kwa kuwa watakuwa wamewasafishia njia ya ubingwa wapinzani wao wakubwa kwenye historia ya soka la Tanzania.
Mwenendo wa timu hizi ukoje?
Kwa mechi tano za hivi karibuni, Simba imeonekana kuwa imara zaidi kwani imeshinda mechi zote, wakati Yanga wameshinda mbili, wametoa sare mbili na kufungwa moja.
Wekundu wa Msimbazi walizitembezea ‘dozi’ Dodoma Jiji, Gwambina, Kagera Sugar, Ndanda FC na Mtibwa Sugar iliyoshukiwa na kichapo kikubwa zaidi cha mabao 5-0.
Katika mechi zake, Yanga wao walizifunga Gwambina (3-1) na Biashara (1-0), huku ikitoa sare mbili dhidi ya KMC a Polisi (1-1), pia ikifungwa na Azam (1-0).
Ukuta v Ushambuliaji
Mara zote matokeo ya mchezo wa soka hutokana na makosa ya safu ya ulinzi na uimara wa washambuliaji wa timu husika.
Ukitazama msimamo wa Ligi, mabeki wa Simba wameruhusu mabao 10, wakati wale wa Yanga wameshapitisha mipira 17 iliyotikisa nyavu zao.
Ukitupia jicho mechi tano za hivi karibuni kwa kila timu, Simba wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja, wakati yanga wamepitisha mabao manne.
Katika hilo, shukrani pekee kwa ‘ukuta’ wa Simba zimuendee kipa Aishi Manula, sambamba na mabeki Shomari Kapombe, Muhamed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango na Paschal Wawa.
Kwa Yanga, yamekuwapo mabadiliko ya safu ya ulinzi kwa siku za hivi karibuni, ukilinganisha na mechi za mwanzoni mwa msimu. Awali, ni Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yasin Mustafa, Bakari Nondo Mwamnyeto na Lamine Moro ndiyo waliokuwa wakicheza mara kwa mara.
Michezo ya hivi karibuni imewashuhudia kipa Farouk Shikalo, Adeyum Saleh, Dickson Daudi na Abdallah Shaibu ‘Ninja wakipata nafasi ya kuonesha uwezo wa kuzilinda nyavu zao.
Ukizungumzia ushambuliaji, Simba imeshaingia kwenye nyavu za wapinzani mara 58, huku Yanga wao wakiwa wametupia jumla ya mabao 41.
Nechi tano zilizopita kwa kila timu zinaonesha kuwa Simba imefunga mabao 12, wakati Yanga wameingia kambani mara sita pekee.
Chama v Carlinhos
Ukweli ni kwamba hii ni vita inayoweza kuifanya ‘derby’ ya kesho kuwa na uhondo wa aina yake pale kwa Mkapa.
Huku kukiwa hakuna shaka juu ya uwezo wa Clatous Chama, kwa mechi za hivi karibuni Carlinhos amekuwa tumaini jipya kwa Wanayanga.
Kama alivyoonesha dhidi ya Azam FC na Tanzania Prisons, Carlinhos ameonesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi (fupi na ndefu).
Tofauti na Feisal Salum ambaye amekuwa akicheza zaidi pasi za nyuma na pembeni, Carlinhos amekuwa ‘direct’ kama alivyo Chama.
Pia, ubora wa wawili hao (Carlinhos na Chama) katika kuingia kupiga wakiwa nje ya boksi ni silaha nyingine kwa kila timu katika dakika 90 za kesho.
Rekodi za ‘derby’ zikoje?
Matokeo ya ‘derby’ za hivi karibuni yanaonesha ugumu wa vita ya kesho pale kwa Mkwapa.
Katika mechi nne zilizopita, kila timu imeshinda moja na mbili zilimalizika kwa sare.
Ndiyo, msimu uliopita, vigogo hao walitoana jasho mara tatu (mechi mbili za Ligi Kuu na moja ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi).
Ukigusa zile za Ligi Kuu, ya kwanza ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, kisha Yanga ikashinda 1-0 kwenye mtanange wa marudiano.
Zilipovaana tena kwenye Mapinduzi, Simba ililipiza kisasi kwa ushindi mnono wa mabao 4-1.
Mechi ya nne ni ile ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo ni sare ya bao 1-1 ndiyo iliyomaliza ubishi.
Kwani makocha wao wanasemaje?
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, amezizungumzia dakika 90 za ‘derby’ ya kesho akianza kwa kusema anaiheshimu Simba kama ilivyo kwa timu zote anazokutana nazo Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Simba ni timu nzuri na naiheshimu lakini siihofii. Kwangu mechi ya Simba haina tofauti na zingine, nafanya maandalizi kama ilivyo kwenye mechi zote,” amesema raia huyo wa Tunisia na Ubelgiji.
Naye kocha msaidizi wa Simba anasema anaupa nafasi kubwa mchezo wa kesho katika mbio za kuifukuzia ‘ndoo’ ya Ligi Kuu Bara.
“Bado tuna nafasi ya ubingwa kwa kuwa tunaongoza kwa pointi nne. Hivyo, kama tutapata ushindi kesho, basi tutakuwa tumepanua wigo,” amesema Matola, kiungo wa ulinzi wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi.