23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Deni la Taifa lafikia Sh trilioni 54

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema hadi kufikia Novemba 30, mwaka jana deni la Serikali limefikia Sh trilioni 54.84 sawa na ongezeko la asilimia 11.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 49.08 Novemba mwaka juzi.

Amesema kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh trilioni 40.39 na deni la ndani ni Sh trilioni 14.44.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Dk. Mpango alisema kuwa ongezeko la deni hilo limetokana na riba ya mikopo ambayo mikataba yake iliingiwa zamani na mikopo mipya yenye masharti nafuu na ya kibiashara ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kukua kwa deni hilo la Taifa kunatokana na sababu kwamba kwa sasa Serikali inalipa madeni ya miaka ya nyuma.

“Kumbukeni fedha ambazo tumekuwa tukikopa tangu uhuru kutoka Benki ya Dunia unaanza kulipa baada ya miaka 40. Na hizi tunazoendelea kukopa watalipa watoto wetu na zimefanya kazi za maana na hicho ndiyo chanzo cha kukua kwa deni kwani tunalipa kwa riba.

“Mahitaji yetu yameendelea kuwa makubwa na fursa za kukopa mikopo nafuu inapungua, tumeanza kukopa mikopo ya kibiashara, lakini tunaanza ile yenye nafuu.

“Lazima tukope, hakuna nchi isiyokopa, hata fedha za mikopo ni za kwetu, kwani za nani? Kwa hiyo tuelewane kile kidogo ambacho tunakopa kina riba, lakini bado tunaenda katika riba ndogo,” alisema Dk. Mpango.

WAHUJUMU WATOA BIL 10/-

Aidha Dk. Mpango alisema hadi Desemba 13, mwaka jana zaidi ya Sh bilioni 10 zimerejeshwa na waliokiri makosa ya uhujumu uchumi.

Hatua hiyo ilitokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli la kutoa wiki moja kuanzia Septemba 22, mwaka jana watuhumiwa wote wenye makosa ya uhujumu uchumi kukiri makosa yao na kuomba radhi na kurejesha kiasi cha fedha wanachoshtakiwa kuhujumu.

Septemba 30 mwaka jana, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga aliwasilisha ripoti ya suala hilo kwa Rais Magufuli na kuongeza kuwa kiasi cha Sh bilioni 107 zitarejeshwa na watuhumiwa hao.

 “Hizi fedha za wale wanaorejesha ambazo walikuwa wamekwapua baada ya fursa aliyotoa Rais (Magufuli) zilifunguliwa akaunti maalumu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka DPP, zipo kwenye akaunti maalumu, huko baadae Serikali ina utaratibu wake itazifanyia maamuzi kwa maana ya matumizi,” alisema wakati akizungumzia kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na tathmini ya awali ya utekelezaji wa bajeti kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20.

UWANJA WA NDEGE MSALATO

Akitolea ufafanuzi kuhusu wananchi ambao wanadai fidia kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, Dk. Mpango alisema wananchi watalipwa na wasiwe na haraka.

“Watalipwa fidia zilizo halali ili ujenzi uanze na sasa fedha tumepata na utakuwa uwanja mzuri na wa kisasa,” alisema Dk. Mpango.

ONYO NOTI BANDIA

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango alisema kuwa watu ambao wanatengeneza na kusambaza noti bandia, kama angekuwa na uwezo wangekatwa miguu na mikono.

“Narudia tena, ni kosa kubwa sana, yaani hawa wanatuhujumu. Ningekuwa ni ‘Law of the Jungle’ na rais wao ni mimi, kwanza ningekata mikono na miguu na kama ni wanaume hata ‘korosho’ zao ningevunja.

“Mnacheka lakini ‘its very serious crime’, angalieni wenzetu Zimbabwe, mpaka mnaanza kutumia sarafu za nchi nyingine, hawa sio watu wa kuwachekea na kuchezea, wanastahili adhabu kali ili wakome na wasirudie, yaani ni jambo kubwa, haiwezekani tupo katika mtumbwi mmoja halafu unatoboa.

“Nawaomba Watanzania mnisikie, kila Mtanzania atambue alama za noti, wengine unakuta hata hiyo saini haifanani na gavana huyu au aliyeondoka. Usiku muwe makini, Mheshimiwa Gavana (Profesa Floreans Luoga) haya masomo muyatoe kwa watu wengine, hii noti ukiiangalia ina kautepe kwa ndani, hizo bandia hazina hiyo,” alisema Dk. Mpango.

RIPOTI YA IMF

Kuhusiana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu hali ya uchumi wa nchi, Dk. Mpango alisema wataipitia tena upya kwani kuna baadhi ya takwimu zilikuwa hazijakaa vizuri.

“IMF tunaenda nao vizuri yale mambo mengine ilikuwa ni baadhi ya wataalamu wa taasisi ile walikiuka maadili, lakini taarifa ile ilikuwa imesambaa sana, wametumia hata uchunguzi maalumu ndani ya IMF lakini ilikuwa ngumu.

“Tulielewana na wamerudi hapa mara mbili na mwezi huu timu ya wataalamu inarudi ili kwa pamoja tupitie tena takwimu mbalimbali za hali ya uchumi wa nchi yetu na dunia kwa jumla.

“Nadhani siku za karibuni tutapokea pia Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha Duniani, yule aliyekuwepo ameondoka.

“Msisitizo wangu kwenu ni kwamba pale ambapo hizi timu zinazungumza nasi, hususan kwenye sekta binafsi waambieni ukweli, msiwape maoni ambayo yameelemea upande mmoja.

“Kama wewe ni wa chama fulani unafanya biashara na huitaki Serikali ambayo ipo madarakani, yaani hata nchi yako hutaki kuisema vizuri tunakushangaa,” alisema Dk. Mpango.

UCHUMI WA TAIFA

Alisema katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka jana, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia  6.8 katika kipindi kama hicho mwaka juzi.

“Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa uwekezaji, hasa katika miundombinu kama vile ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege, kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, kuimarika kwa huduma za usafirishaji, kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hasa dhahabu na makaa ya mawe,” alisema Dk. Mpango. 

Alisema sekta zilizokua kwa kasi kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka jana ni pamoja na ujenzi (16.5%), uchimbaji madini na mawe (13.7%), habari na mawasiliano (10.7%), maji (9.1%) na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (9.0%).

MFUMUKO WA BEI

Alisema mfumuko wa bei uliendelea kubakia ndani ya lengo la asilimia 5.0 katika mwaka ulioishia Novemba 2019, ambapo katika kipindi hicho, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 ukilinganishwa na asilimia  3.0 katika kipindi kama hicho mwaka juzi.

“Kiwango hiki ni chini ya lengo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki la asilimia 8.0,” alisema Dk. Mpango.

Alisema Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka huu na kwa wastani wa asilimia 7.1 katika kipindi cha muda wa kati.

Alisema Maoteo hayo yamejengwa katika misingi ya Uendelezaji wa uwekezaji katika miradi ya miundombinu na utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara.

Dk. Mpango alisema zipo changamoto mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kukabiliana nazo kwa kushirikiana na wadau, hususan sekta binafsi ambazo ni uwezekano wa kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la dunia.

Alizitaja  changamoto zingine ni athari za vita ya kiuchumi baina ya mataifa makubwa kiuchumi (hususan Marekani na China) na kuongezeka kwa gharama za mikopo.

GAVANA ATOA NENO

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Floreans Luoga,  alisema suala la noti bandia wamekuwa wakilishughulikia kwa kina.

“Hilo tunalifuatilia, ndiyo maana ndani ya benki hakuna fedha bandia, mtu yeyote anayehusika na utengenezaji, huyo anataka kuleta maafa makubwa kwa nchi.

“Na mara ya mwisho  wakati nalizungumzia hili, nilisema turudi kwenye adhabu za kijamii ambazo ni kumtenga na jamiii na kumfukuza akaishi kwenye uhayawani wake,” alisema Profesa Luoga.

KUTUMA, KUPOKEA FEDHA

Akilitolea ufafanuzi suala la kutuma na kupokea fedha katika mitandao ya simu, Profesa Luoga alisema kuwa Serikali inakuja na mfumo mmoja ili kuhakikisha gharama zinakuwa chini.

“Unapotuma fedha yule anayehamisha mpaka kukufikia wapo wengi, kitu kinachofanyika ni kutekeleza uanzishwaji wa ‘National Switch’, tuna ‘syteam’ tunaijenga kwa sasa itaondoa hawa wote wa katikati na itakapokamilika hakutakuwa na gharama kubwa ili utumaji, upokeaji wa fedha uwe ni nafuu kabisa,” alisema Profesa Luoga.

UTAKATISHAJI WA FEDHA

Kuhusu utakatishaji wa fedha, Profesa Luoga alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana nao.

“Hilo ni kosa na hatua zimeendelea kuchukuliwa kuhakikisha utakatishaji fedha haufanyiki na watu wengi wameingia katika matatizo na wapo mahakamani,” alisema Profesa Luoga.

RIBA KUBWA

Kuhusiana na riba kubwa zinazotolewa na taasisi ndogo za kifedha, Profesa Luoga alisema sio sawa na Serikali inakuja na mfumo maalumu wa kudhibiti.

 “Sio sahihi kwa mabenki kupeleka gharama za uendeshaji kwa wateja, hatua mbalimbali tumezichukua ikiwemo riba kushuka na riba tunataka iwe chini na zikizidi kuwa juu tutachukua hatua na tumeanza kuchukua hatua kwa kuzifanyia uchunguzi na tutachukua hatua,” alisema Profesa Luoga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles