23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

‘Demokrasia itaendelea kuheshimiwa nchini’

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

SERIKALI imesema kuwa inaendelea na kazi ya kuimarisha demokrasia kwa wananchi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura ambazo zitatumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Hayo yalisemwa jana na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbasi.

Dk. Abbasi aliwaongoza makatibu wakuu jijini Dodoma kuhakiki na kuhuisha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura ambapo jana ilikuwa mwisho wa uhakiki wa taarifa nchini.

 “Serikali inaendelea kukamilisha kuboresha daftari la kudumu la mpigakura, Serikali inatambua kwamba kazi hii ni muhimu sana kwa nchi yetu ikizingatiwa ni la kidemokrasia licha ya kwamba nchi yetu na dunia nzima inapitia kwenye changamoto tuliyonayo ya Covid-19,” alisema Dk. Abbasi.

Alisema kuwa demokrasia itaendelea kuheshimiwa nchini kwa sababu ni kitu muhimu sana na kuwataka viongozi hao pamoja na wananchi waliojiandikisha kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wao. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, alisema kuwa wizara yake ina jukumu la kuhamasisha mambo mbalimbali ikiwemo elimu ya haki ya mpigakura.

“Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika demokrasia kiasi kwamba tunajivunia hatua tuliyofika ni nzuri na demokrasia imekuwa ni ya kweli, hakuna mwaka ambao tumevuka miaka mitano hatujafanya uchaguzi na wanannchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wao,” alisema Profesa Mchome.

Alisema lengo la elimu ya mpigakura ni kuwahamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza na kushiriki kuchagua viongozi wao watakaowaongoza ili kujenga demokrasia na utawala bora nchini.

Profesa Mchome alisema hatua hiyo inaanza kwa wananachi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpigakura ambalo linaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles