23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DEGEDEGE: UGONJWA USIOCHAGUA RIKA

 

Na MWANDISHI WETU,

DEGEDEGE ni hali ya ghafla ya kutingishika mwili mzima au mikono na miguu kunakosababishwa na kukakamaa kwa misuli ya mwili.

Tatizo la degedege mara nyingi linatokana na magonjwa au hitilafu katika ubongo ambapo husababisha kutokea kwa  upungufu wa vichocheo vya sukari kwenye damu (Hypoglycemia) pamoja na upungufu wa hewa ya oksijeni kwenye damu (Hypoxia).

Mwaka 2013 ugonjwa huu uliua zaidi ya watu laki moja duniani, huku asilimia 80 wakiwa Waafrika.

Hata hivyo, maradhi haya husababishwa na magonjwa mbalimbali na mara nyingi hujitokeza kwa watu ambao wana familia yenye historia ya ugonjwa huu au kifafa.

Watu wa rika zote wanaweza kuathiriwa na degedege, lakini watoto na vijana ndio huathirika zaidi na inapojirudia huitwa kifafa.

Imani za kuwa mtu mwenye degedege hachomwi sindano zimechangia kuongezeka kwa vifo au mtindio wa ubongo ambavyo hutokea iwapo  maradhi haya hayakutibiwa kwa haraka na kwa ufasaha.

Wakati mwingine si rahisi kubaini iwapo mtu amepatwa na degedege kutokana na baadhi ya watu hushikwa na bumbuwazi (kuduwaa) kwa muda mfupi hivyo kutojua kama amepatwa na degedege au la.

Dalili

Wataalamu wa afya wanasema dalili za maradhi haya hutegemea sehemu ya ubongo ambayo imeathirika na hujitokeza kwa haraka ambapo husababisha mwili, miguu na mikono kuanza kukakamaa na kurudisha kichwa nyuma.

Kushindwa kupumua na kutokwa na mapovu mdomoni, macho kugeukia nyuma na kuonekana kwa sehemu nyeupe ya jicho.

Kupoteza fahamu au kuzimia ikifuatiwa na kuchanganyikiwa (mgonjwa anapoteza kumbukumbu) pamoja na kushindwa kuzuia mkojo na haja kubwa.

Hata hivyo, shambulio la degedege huisha baada ya muda mfupi mara nyingi chini ya dakika tano.


 Baada ya shambulio hupitiwa na usingizi mzito kama takribani dakika 30 hadi saa nzima na azindukapo hushindwa kutambua kitu chochote kwa muda.

Chanzo chake

Degedege si ugonjwa bali ni maradhi yanayosababishwa na magonjwa mbalimbali,pia hutokana na  kuvurugika kwa mfumo wa umeme katika ubongo.

Chanzo kikubwa cha degedege hutokana na maambukizi kwenye ubongo na uti wa mgongo.

Kuumia ubongo kunakoweza kujitokeza wakati wa  kujifungua, ugonjwa wa malaria, homa kali hasa kwa watoto, kifafa pamoja na kifafa cha mimba.

Matibabu

Matibabu yake hutegemea chanzo cha maradhi hayo, mfano iwapo degedege imesababishwa na malaria au homa ya uti wa mgongo, mgonjwa anapaswa kutumia dawa za kutibu malaria na antibiotiki.

Pia mgonjwa huweza kutumia dawa zinazosaidia kudhibiti degedege

Madhara

Mwenye degedege asipopata tiba sahihi kwa wakati anaweza kupatwa na madhara yafuatayo: 
1. Kupata tatizo la kifafa, mtindio wa ubongo kwa watoto inaweza kuchangia uelewa duni katika masomo yake.

Ukuaji duni kwa mtoto hasa kama degedege ikiwa itamtokea mara kwa mara hatimaye mtoto kudumaa.

Inashauriwa na wataalamu wa afya kuwa pindi mtu apatapo degedege kuwahishwa haraka katika zahanati ili kumwepushia kupata magonjwa ambayo yanaweza kumsababishia magonjwa ya kudumu katika maisha yake.

Makala haya imeandaliwa kwa msaada wa mitandao

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles