30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

DED, wataalamu wapewa maagizo mazito Rorya

Na Peter Fabia -Rorya

MKURUGENZI na wataalamu wa Halmashauri ya Rorya, wameagizwa kutekeleza upelekaji wa fedha za maendeleo asilimia 20 ya kila mwaka katika kata 26 za wilaya hiyo.

Agizo hilo lilitolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya.

Hatua hiyo, ilitokana baadhi ya wajumbe kutaka Kiboye amuulize Mkurugenzi wa Rorya, Charles Chacha kwanini ameshindwa kupeleka fedha kata zote 26 kwa miaka minne sasa.

“Mkurugenzi peleka fedha, ni sheria ndiyo inavyosema na si kukaa nazo, wananchi wanahitaji maendeleo, madiwani hamuwatendei haki wananchi kwa kushindwa kusimamia wataalamu,” alisema Kiboye.

Mbunge wa Rorya, Lameck Airo (CCM), aliwahasa wataalamu kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kiwango na kuwezesha wananchi kupata huduma muhimu, badala ya kuchakachua fedha.

Alisema wamegundua mradi wa majisafi wa zaidi ya Sh milioni 500 katika Kata ya Bukwe umeshindwa kutoa huduma,licha ya kudaiwa kukamilika kwa miezi nane sasa.

“Mradi huu umekataliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Mzee Mkongea Ali alipotaka kuuzindua kwa madai ujenzi wake upo chini ya kiwango, umeshindwa kuhudumia wananchi hii ni kero ndani ya jimbo letu,” alisema Airo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Charles Ochere alimuomba  Chacha ambaye aliwakilishwa na kaimu mkurugenzi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi wa Halmashauri, Joseph Jumbe kumchukulia hatua kali za kinidhamu, ikiwamo kumkamata Mtendaji wa Kata ya Kirogo, Ernest Magesa aliyetoroka kwa muda wa mwezi mmoja sasa na Sh milioni 1.2 za wananchi, walizochanga kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maendeleo wa ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari ya kata hiyo.

Kwa upande wake, Jumbe aliwahakikishia viongozi hao na wajumbe wa kikao hicho watayafanyia kazi maagizo yaliyotolewa, huku akiahidi kutumia vyombo ulinzi na usalama kumsaka na kumkamata  Magesa aliyetoroka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles