Na Lushishi Robert, Serengeti
TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara, imemfikisha mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Goody Kitambo kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababisha Serikali hasara ya Sh milioni 24.5.
Kitambo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti akituhumiwa kwa kosa la kutumia vibaya madaraka yake ikiwa ni pamoja na kukiuka sheria ya ununuzi wa umma kwa kuelekeza magari ya halmashauri ya wilaya hiyo kufanyiwa matengenezo katika karakana binafsi ambazo hazijaidhinishwa na Serikali kinyume cha kifungu cha 59 (1) ya sheria ya ununuzi wa umma.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Amoni Kahimba, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Marshal Mseja, akisaidiana na Martin Makani waliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa kwa nyakati tofauti amekuwa akivunja sheria na kanuni za ununuzi wa umma ya mwaka 2005.