De Jong awaomba radhi Barcelona

0
1022
Frenkie de Jong

BARCELONA, HISPANIA

KIUNGO wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Hispania, Barcelona, Frenkie de Jong, amewaomba radhi mashabiki baada ya kuoneshwa kadi nyekundu juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Espanyol.


Mchezo huo ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2, huku bao la pili la Espanyol likipatikana baada ya nyota huyo wa Barcelona kuoneshwa kadi nyekundu katika dakika ya 75 na bao kupatikana dakika ya 88.


Baada ya De Jong kuoneshwa kadi hiyo mchezo ulionekana kuwa mgumu kwa upande wa Barcelona hasa katika eneo la katikati mipira ikipotea kwa urahisi, huku mashabiki wakiamini kama mchezaji huyo angeendelea kuwepo basi wapinzani wao wasingepata bao hilo la kusawazisha.


Awali De Jong alikuwa na kadi ya njano, lakini alijisahau na kwenda kumchezea vibaya nyota wa timu hiyo Jonathan Calleri, jambo ambalo lilimfanya aonyeshwe kadi nyingine ya njani ya pili na kisha nyekundu.


Hata hivyo, historia yake ya kadi nyekundu imeanzia kwenye mchezo huo, tangu aanze kucheza soka la kulipwa hajawahi kuonesha kadi nyekundu, hiyo ndio mara yake ya kwanza. Kutokana na hali hiyo mchezaji huyo amewaomba radhi mashabiki zake kwa kitendo cha kijinga alichokifanya.


“Nilikosa umakini kwenye mchezo huo, sikutarajia kuoneshwa kadi yoyote, lakini kutokana na makosa niliyoyafanya nikaadhibiwa, limekuwa pigo kwa klabu yangu, limekuwa pigwa kwangu pia, jambo ambalo linaniumiza.


“Nimeikosea timu, nimewakosea mashabiki, lakini ni jambo ambalo linatokea uwanjani, kuna kitu kikubwa ambacho nimejifunza kutoka kwenye mchezo huo, hivyo naomba radhi mashabiki pamoja na viongozi wa timu kwa kilichotokea,” alisema mchezaji huyo.


Kutokana na sare hiyo, Barcelona kwa sasa bado inaendelea kuongoza kwenye msimamo wa Ligi huku ikiwa na pointi 40 baada ya kucheza michezo 19, lakini wapo sawa na wapinzani wao Real Madrid, ila tofauti yao ni idadi ya mabao, Barcelona wakiongoza kwa mabao mengi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here