MANCHESTER, ENGLAND
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Manchester City, Kevin de Bruyne, huenda akaukosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Celtic, baada ya kupata jeraha katika mchezo dhidi ya Swansea ambapo timu yake ilipata ushindi wa mabao 3-1.
Mbelgiji huyo mwenye thamani ya pauni milioni 56, jana alitarajia kufanyiwa uchunguzi wa jeraha lake baada ya kulalamika maumivu makali ya mguu katika mchezo huo.
Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola, hajawa na wasiwasi kumkosa nyota huyo wakati wakisafiri kuelekea jijini Glasgow, Scotland.
Kocha huyo alisema kutokana na namna ambavyo nyota wake alivyokuwa akilalamika, inaonekana wazi alipata jeraha ya nyama za paja.
“Sijajua jeraha hilo litakuwa kubwa kwa kiasi gani kwa kuwa mimi si daktari, tukifika Manchester atapatiwa uchunguzi ili kufahamu kitu kinachomsumbua.
“Nasikitika sana kwani Kevin ni mchezaji muhimu katika timu yetu, hiyo ndio sababu ya kuwa na kikosi kipana,” alisema Guardiola.
Manchester City iliwafunga kwa mara ya pili ndani ya wiki moja timu ya Swansea baada ya kuwafunga mara ya kwanza katika mchezo wa Kombe la Ligi ya England (EFL).
Mshambuliaji wa timu hiyo, Sergio Aguero, alifunga mabao mawili katika mchezo huo wa EFL.
Aguero kwa sasa amefunga mabao 11 katika michezo sita msimu, huu hata hivyo Guardiola anataka nyota huyo kujituma zaidi uwanjani.
Kocha huyo alimpongeza nyota huyo baada ya ushindi huo na kumweleza kuwa anaweza kufanya vizuri zaidi ya ushindi wa mabao hayo.