24.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 7, 2021

DCI: Tulieni nitatoa taarifa uchunguzi wa dhahabu

BENJAMIN MASESE -MWANZA

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amewasili jijini hapa na kuzuia kiongozi yeyote kuzungumzia ukamataji wa dhahabu hadi atakapomaliza uchunguzi wa suala hilo.

DCI Boaz  aliwasili mkoani hapa juzi,  ikiwa ni siku moja baada ya polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kukamata wafanyabiashara watatu wakiwa na dhahabu ya uzito wa kilo 323.6 na fedha Sh milioni 305 ambazo hadi sasa hazijaelezwa zilikuwa zinapelekwa wapi.

Agizo la DCI Boaz limekuja kukiwa na taarifa za uhakika kuwa polisi saba  waliohusika kuwakamata watuhumiwa  hao wamewekwa chini ya ulinzi  wakichunguzwa kwa kile kilichodaiwa  hawakutimiza wajibu wao kutokana na maadili ya kazi yanavyoelekeza.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna, alisema awali suala hilo lilikuwa linashughulikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, lakini baada ya kuwasili Boaz litakuwa  chini yake.

 “Jana (juzi) nilikwambia mkuu wa mkoa ndiye msemaji wa jambo hili, mambo yote yanayoendelea, baada ya kiongozi wetu DCI kuwasili hapa, maelekezo ni kwamba yeye ndiye atatoa mwongozo nani wa kusema pale atakapomaliza kulifanyia kazi.

“Inawezekana akanipa mimi ruksa ya kusema au mkuu wa mkoa au yeye mwenyewe, kikubwa jambo hili linashughulikiwa kwa nguvu kubwa na muda ukifika mambo yatawekwa wazi mbele ya vyombo vya habari.

“Hivyo nakuomba na waambie waandishi wenzako muwe na subira, tumwache kiongozi wetu atimize majukumu yake bila kusumbuliwa.

“Yapo mambo mengi yanasemwa katika sakata hili na mengine yanaandikwa  na kutangazwa kwenye vyombo vya habari, yapo ya kweli na yapo mengine ni vigumu kuyathibitisha, tuvute subira taarifa itakuja rasmi,” alisema.

KAMISHNA MKUU TRA

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charels Kichere naye amewasili mjini hapa na kufanya vikao na baadhi ya viongozi wa Serikali.

MTANZANIA ambalo lilifika ofisi za TRA kwa lengo la kupata taarifa za suala hili kama lilivyoahidiwa juzi na Meneja wa mamlaka hiyo Mkoa wa Mwanza, Ernest Dundee, lilimshuhudia Kamishna Kichere akiwa na viongozi wengine katika kikao.

Chanzo chetu kilidokeza kuwa miongoni mwa ajenda zilizokuwa zikijadiliwa katika kikao hicho ni kuona kama wafanyabiashara hao walikuwa wanalipa kodi stahiki na mambo mengine.

Hata hivyo, jitihada mbalimbali za kumpata Dundee ili kuelezea viongozi waliofika katika ofisi na lengo la kikao hicho zilishindikana baada ya simu yake kuita bila kupokewa na mara nyingine ilikatwa au kuzuiliwa.

Ilielezwa baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Madini na taasisi zake walihudhuria kikao hicho.

Kwa upande wake, Mongela alipotafutwa kwa nyakati tofauti hakupatikana na taarifa kutoka ofisini kwake zilidai alikwenda katika kikao  cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally.

Tukio la kukamatwa dhahabu na fedha, lilitokea Januari 5, mwaka huu eneo la Kivuko cha Busisi kilichopo Wilaya ya Misungwi, baada ya taarifa kutoka kwa raia mwema walizotoa kwa Jeshi la Polisi.

Watuhumiwa hao walikuwa wakitumia magari mawili, moja likiwa limebeba dhahabu na jingine fedha. Magari hayo ni Toyota Mark 11 yenye namba za usajili T 208 DCT na Kluger T 726 DPJ.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema baada ya kupata taarifa waliandaa mtego na kufanikisha kuyazuia magari hayo na kikosi kazi cha polisi kiliweza kufanya upekuzi na kukuta na pesa na dhahabu hiyo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,400FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles