24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

DC WILAYA YA TANGA AWAONYA WANASIASA

 

Na AMINA OMARI-TANGA

MKUU wa Wilaya ya Tanga, Tobias Mwilapwa, amevionya vyama vya siasa vinavyotarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wilayani hapa, vifanye kampeni za amani ili kuepuka vurugu.

Mwilapwa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

Kwa mujibu wa Mwilapwa, kampeni za amani ndizo zitakazoendelea kuweka amani wilayani hapa kwa sababu bila amani hakuna shughuli za maendeleo zitakazofanyika.

“Kama mnavyojua, ni kwamba hapa wilayani Tanga tuna uchaguzi katika kata mbili ambao utafanyika sambamba na kata nyingine nchini ambazo nazo zina chaguzi ndogo.

“Kwa hiyo, nawaomba wanasiasa kupitia vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo, wawe makini saa zote wakati wa kampeni ili kuepuka uvunjifu wa amani.

“Pia, napenda kuwahakikishia wananchi wote, kwamba vyombo vya usalama vimejipanga kuhakikisha amani inakuwapo wakati wote wa uchaguzi huo kwa sababu hatutaki kushuhudia vurugu za aina yoyote,” alisema Mwilapwa.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya alisema  Jeshi la Polisi wilayani hapa linaendelea kuchunguza matukio yote ya uhalifu ambayo yamekuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali wilayani hapa.

“Hivi karibuni yametokea matukio matatu ya wananchi kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao pamoja na tukio moja la kihalifu lililosababisha kifo cha mtu mmoja.

“Kwa kushirikiana na kamati yangu ya ulinzi na usalama, tumefanikiwa kuwakamata watu kumi ambao inasemekana walihusika kwenye matukio hayo ya uporaji katika kata za Magaoni na Masiwani wilayani hapa.

“Pamoja na hayo, nawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano ili tuendelee kukabiliana na wahalifu wanaotishia ukosefu wa usalama katika wilaya yetu,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles