24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

DC Muleba amtaka Mkandarasi wa REA kukamilisha mradi kwa wakati

Na Renatha Kipaka, Muleba

Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila na Wajumbe wa Kamati ya Usalama wa wilayani humo wametembelea na kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme wa REA awamu ya tatu katika ijiji vya Bweyenza, Kangoma na Nyakashenye vilivyopo kata ya Mubunda wikayani humo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Juni 21, 2022 amemtaka Mkandarasi kumaliza kazi kwa mapema ili wananchi waweze kupata umeme.

Nguvila amemsisitiza Mkandarasi huyo kuwa kiu ya wananchi ni kupata umeme hivyo anatakiwa kuhakikisha anakamilisha mradi mzima kwenye vijiji vyote 30 ndani ya muda aliopewa katika mkataba pasipo kuvuka miezi sita waliyobakiza.

“Nitumie fursa hii kusema kuwa ndani ya siku 14 kwa wale wote ambao watakuwa karibu na nguzo wawashiwe umeme ili waanze kunufaika na umeme kwa sababu mmenieleza kuwa vifaa vipo, nguzo nimeziona na nyaya zipo, hivyo wananchi kazi yenu ni kuunga nyaya majumbani ili wanapofika hapa wanakuwekea mita ili kuanza kupata huduma ya umeme,” amesema Nguvila.

Aidha, amemuelekeza Mkandarasi kutoa taarifa kwa wananchi endapo kuna ukataji wa miti, migomba, mibuni na mazao mengine kwenye maeneo ambayo wanapitisha nguzo/kwenye njia za kupitisha nguzo ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Sambamba na hayo amemtaka Mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anawalipa vibarua stahiki zao kwa wakati huku akiwataka vibarua nao kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kazi iishe kwa wakati.

Nae Mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Padon Emmanuel amesema kuwa ndani ya siku 14 vijiji vya Bweyenza, Kangoma na Nyakashenye watawashiwa umeme huku akiahidi kumaliza mradi kwa vijiji vyote 30 ndani ya miezi sita kama alivyosaini katika mkataba.

Mkazi wa Kijiji cha Kangoma, Jackson Thadeo amesema kuwa baada ya kupata umeme itawasaidia kunufaika na umeme huo kwa kueleza kuwa watafungua vibanda vya kunyolea nywele na kazi mbalimbali za kuwaingizia kipato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles