|Suzan Uhinga, Tanga
Mkuu Mpya wa Wilaya ya Korogwe, Kisa Gwakisa, ameahidi kupambana na vitendo vya rushwa na ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo.
Amesema atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake ili kuziba mianya ya rushwa wilayani humo.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hayo muda mfupi baada ya kuapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kuongeza kuwa hatafumbia macho vitendo vyovyote vinavyoashiria rushwa kwa mustakabali wa wilaya hiyo.
“Nitahakikisha napambana na wala rushwa na watoa rushwa na kama wapo basi wajiandae maana sitalifumbia macho suala hili ambalo linakwamisha shughuli za maendeleo,” amesema Kisa.
Pamoja na mambo mengine, amesema mbali na vipaumbele hivyo pia katika utendaji wake atakomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na watoto ili kuweka usawa na amani kwenye jamii atakayoiongoza.
“Suala jingine nitahakikisha nakomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwenye jamii pamoja na ukatili dhidi ya watoto hili nitalivalia njuga nikiwa kama mama na kiongozi wa umma,” amesema.