27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DC Mmanda kuzikwa na wachache Mtwara

NA FLORENCE SANAWA-MTWARA

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda anatarajiwa kuzikwa mkoani hapa huku Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa akitoa utaratibu wa maziko hayo na kusisitiza kuwa hakutakuwa na mikusanyiko yoyote na watu watakaohudhuria maziko hayo hawatafika 10.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Byakanwa alisema kuwa Mmanda alifikwa na umauti juzi usiku akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula ambako alikuwa akitibiwa maradhi ya kisukari pamoja na shinikizo la damu.

Alisema kuwa baada ya kuwasiliana na familia yake, utaratibu umepangwa kuwa maziko yatafanyika mkoani Mtwara ambapo yatahudhuriwa na watu 10 ili kuepuka msongamano na mikusanyiko ya watu kama njia ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona.

“Ni kweli Mmanda amefariki, alilazwa Ligula na ilipofika Jumamosi hali ilibadilika na kufikwa na umati Jumapili saa 5 usiku. Kutokana na hali halisi ilivyo pamoja na katazo la kuweka mikusanyiko nchini, tunalazimika kusimamia msiba huu na kuhakikisha kuwa wanahudhuria watu 10 tu.

“Maziko yote yatafanywa na Serikali na atazikwa hapa hapa Mtwara baada ya kukubaliana na familia yake, tuko katika wakati mgumu, lazima tuzingatie utaratibu wa afya na taratibu za kiserikali na za kiutumishi wa umma kama inavyotakiwa.

 “Mmanda alikuwa shupavu, mfanyakazi aliyekuwa anajitoa kila mara pale inapohitajika, apumzike kwa amani, ni kwavile tu hatuwezi kukusanyika kutokana na tahadhari ya corona, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi ameni,” alisema Byakanwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara Mjini, Seleman Mpilu, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za msiba kwa mshituko mkubwa.

“Tulipokea taarifa alfajiri kuwa mkuu wetu wa wilaya amefariki, tumeumia, tumesikitishwa sana. Alikuwa ni mjumbe wetu, hatuna budi kumuombee kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi,” alisema Mpilu.

Kwa upande wao, mwananchi wa Mtwara, Shabani Hamis amesema kuwa wamepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha Mkuu huo wa wilaya.

Naye Asha Seleman, alisema kuwa taarifa za kifo cha mkuu huyo wa wilaya zimekuwa za mshtuko kwani nao kama wananchi walipenda kushiriki hatua zote za msiba huo, lakini kutokana na tahadhari iliyotolewa wanaamini watawakilishwa vyema na watakaopata nafasi ya kushiriki maziko hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles