*Lori lakamatwa likijiandaa kubeba mafuta ya wizi, dereva akimbia
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amevitaka vyombo vya dola katika wilayani humo kuwasaka watu wote waliopanga njama ya kutaka kuiba mafuta aina ya dizeli katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR katika mji wa Malampaka wilayani humo.
Akizungumza Agosti 4, mwaka huu katika eneo la kupondea kokoto la mradi huo ambapo Lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 766 DJD mali ya kampuni ya OCHELE SERVICE STATION LTD (OSS) ya wilaya ya Rorya mkoani Mara kukamatwa likiwa katika maandalizi ya kufanya wizi huo kabla ya kukurupushwa na Askari polisi wa reli waliokuwa kwenye doria nyakati za usiku.
Gari hilo lilikamatwa saa nane usiku wa kuamkia Agosti 4, mwaka huu na dereva wa gari hilo kutoroka lakini eneo ambalo mafuta hayo yalikuwa yamehifadhiwa kwenye tenki la mradi huo lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 mageti yote yalikuwa wazi na kufuli la kuingilia eneo la tenki nalo lilikuwa wazi na baada ya jaribio kushindwa kufanikiwa walinzi wa eneo hilo walitoroka.
Amesema ukiangalia kwa ujumla tukio zima utagundua ni njama ambayo imepangwa na kuhusisha watu mbalimbali kuhujumu mradi wa kimkakati wa kitaifa na sehemu yao ni wale waliopewa dhamana ya kusimamia na kutekelwza mradi huo.
“Ukiangalia hili tukio siyo la kawaida, haiwezeka gari hili linapota eneo lote la mradi hadi hapa kwenye eneo la kisima ambapo kuna matenki ya kuhifadhia mafuta bila kuzuiwa, ni wazi hap kuna mlolongo wa watu katika jambo hili na wengine ni wale waliopewa dhamana ya ujenzi na ulinzi wa mradi huu hili jambo haliwezekani kila siku tunapambana na wizi lakini bado wanaendelea ni lazima hatua zichukukiwe sasa kwa wahusika.
“Ni vizuri uchunguzi ufanyike kwa kina ili kubaini watu wote waliohusika kufanya njama ya tukio hili na yeyote atakayebainika kupindisha au kupotosha taarifa ya tukio hili atachukuliwa hatua kali za kisheria, pia naagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mmiliki wa Lori hilo ambalo lina uwezo wa kubeba lita 30,000 za mafuta,” amesema Kaminyonge.
Aidha, amewataka wananchi na watu wote waliopewa dhamana ya ujenzi na usimamizi wa mradi huo kulinda mali zote za mradi huo kwani unatumia fedha za walipa kodi wa nchi hii ili kukomesha wizi huo.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia tukio hilo wamesema kuwa haiwezakani gari hilo kuingia kwenye eneo la mradi ambalo ni umbali mrefu huku kukiwa na walinzi maeneo yote lakini liliweza kupita hadi kufika eneo la tanki na kueleza kuwa hizo njama zinahusisha vigogo wakiwemo wengine kwenye serikali na vyombo vya dola viliopewa dhamana ya ulinzi wa mali xa mradi huo na kuomba uchunguzi ufanyike wa kina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Bladius Chatanda amesema hadi sasa watu watano wamekamatwa na jeshi hilo kuhusiana na tukio hilo kwa mahojiano zaidi.
Kamanda Chatanda amewataja waliokamatwa kuwa ni Gerald Mgaya, Joseph Isack ambao ni Maafisa Usafirishaji wa Kampuni ya ujenzi ya CCECE, Hanjia Fang raia wa China ambaye ni msimamizi wa eneo la kupondea kokoto, Charles Ochelle mmiliki wa gari hilo na Stephen Ndaki ambaye ni Mfanyabiashara wa jijini Mwanza.