Na Clara Matimo, Ukerewe
Jumla ya ekari 193 za ardhi katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza zimefanikishwa kurudishwa katika umiliki wa serikali kutoka kwenye familia iliyokuwa inazimiliki awali baada ya Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Denis Mwila kufikia makubaliano na familia hiyo.
Ekari hizo ambazo ziko Kijiji cha Galu kata na Tarafa ya Ilangala, zilikuwa zinamilikiwa na familia ya Masatu Kezilahabi ambaye kwa sasa ni marehemu kinyume na sheria hali iliyosababisha kuibuka kwa mgogoro wa ardhi baina yake na Serikali ya kijiji hicho ingawa ulitatuliwa mwaka 2019 na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Colnel Magembe.
Akizungumza hivi karibuni baada ya kutembelea eneo hilo na kutatua mgogoro huo, Kanali Mwila amesema alipokea malalamiko ya mgogoro huo kutoka kwa viongozi wa Kijiji hicho na kuamua kufika eneo hilo ili kujionea hali halisi ambapo alifanya kikao cha ndani na kamati ya usalama ya wilaya, wataalam wa idara ya adrdhi mwanasheria wa halmashauri, wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Galu, Diwani wa kata ya Ilangala, watendaji wa kata hiyo na mlalamikaji, Obedi Masatu (mtoto wamarehemu Masatu Kezilahabi).
Ameeleza kuwa Septemba 3, 2019 kulifanyika utatuzi wa mgogoro wa ardhi hiyo mbele ya kikao cha hadhara kilichowahusisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Colnel Magembe, kamati ya usalama ya wilaya, wajumbe wa serikali ya Kijiji, wataalam mbalimbali ndani ya Kijiji na kata hiyo na wananchi wa kijiji hicho ambapo Marehemu Kezilahabi alituhumiwa kujimilikisha eneo la ekari 200 za shamba la halmashauri ya kijiji hicho kinyume na sheria.
Katika kikao hicho marehemu Kezilahabi alikiri kujimilikisha ekari 200 na hivyo alikubali kuzirejesha huku akitoa ombi kwa serikali ya kijiji imsaidie ekari saba ambazo zilikuwa zimepandwa miche ya michungwa na mihogo kwa shughuli za kifamilia ambapo ombi hilo lilikubaliwa na Kezilahabi kusaini mkataba wa makubaliano.
Pia Mzee Kezilahabi aliridhia kubomoa nyumba mbili alizojenga katika ardhi hiyo na kuikabidhi kwa uongozi wa kijijini lakini baadaye mtoto wake (Obed) ambaye ni msimamizi wa mirathi ya Kezilahabi na hakuwepo katika kikao hicho alizuia serikali ya kijiji kukata miti na kutumia mawe yaliyokuwa kwenye shamba hilo kwa ajili ya shughuli za ujenzi hivyo uongozi wa Kijiji cha Galu kupeleka malalamiko kwa Mkuu wa Wilaya.
Hata hivyo, kikao hicho kilichofanyika katika shule ya sekondari ya Ilangala kwa takribani saa mbili pande zote mbili zilikubaliana kwamba eneo lenye ukubwa wa ekari 193 lililokuwa likimilikiwa kinyume na sheria na familia hiyo litabaki kuwa mali ya serikali ya Kijiji hicho na kutumiwa na wananchi kwa maendeleo ya kijiji.
Diwani wa Kata ya Ilangala, Bituro Misana amemshukuru mkuu wa Wilaya kwa hatua hiyo ya utatuzi wa mgogoro huo uliodumu kwa kipindi kirefu na kurejesha ardhi hiyo ambayo sasa itatumika kwa shughuli za maendeleo za kijiji cha Galu pamoja na kuleta amani kwa wakazi wa eneo hilo.