Na Denis Sinkonde, Songwe
Mkuu wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Anna Gidarya amewataka wadau wanaosafirisha abiria kwa kutumia vyombo vya moto kutoka Ileje Mpemba hadi Mbeya kuacha kuwatoza nauli kubwa abiria kinyume na nauli elekezi kutoka(LATRA), hivyo wasubiri maagizo kutoka kwenye Mamlaka hiyo.
Gidarya ameyasema hayo Aprili 20, 2022 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake kutokana na malalamiko ya wananchi wanaosafiri kutoka wilayani Ileje kuishia baadhi ya vituo ndani ya wilaya na kutoka Ileje kwenda Mbozi, Momba na Mkoa wa Mbeya kulalamikia kupanda kwa nauli kiholela kutoka Sh 2,000 ya awali mpaka 3,000 kwa sasa.
Gidarya amesema kupanda kwa nauli kumepelekea baadhi ya wananchi kushindwa kusafiri kutokana na kutokuwa na nauli ya kwenda na kurudi kutoka mpemba Sh 4,000 ya awali na nauli ya sasa ni Sh 6,000 kwenda na kurudi.
“Wamiliki wa vyombo vya moto pamoja na waajiri (maderva) wawe na subira ya kusubiri tamko la Mamlaka ya udhibiti wa usafiri Aridhini (LATRA) watakapotangaza maelekezo mengine kama ni bei mpya za nauli au kubaki zile za awali.
“Ninawaagiza askari wa usalama barabarani wakiongozwa na mkuu wa usalama barabarani wilayani humo (DTO) kufanya ukaguzi wa maderva ambao wamepandisha nauli kiholela bila kusubiri utaratibu wa Mamlaka husika,” amesema Gidarya.
Aidha, Gidarya alisema anatarajia kuitisha kikao na wadau wa usafirishaji pamoja na wamiliki wa vyombo vya moto kujadiliana na kupokea changamoto Katika kipindi hiki ambacho kimekuwa na changamoto kwa upande wa abiria na wadau hao.
Baadhi ya madereva wanaofanya safari za kusafirisha abiria kutoka Itumba wilayani Ileje mpaka Mpemba wilayani Momba wamesema tatizo la kupandisha nauli kutoka Sh 2,000 mpaka 3,000 no kutokana na kupanda kwa Bei ya nishati ya mafuta hali ambayo imekuwa changamoto kutoza nauli 2,000 kwani imekuwa hasara.
“Katika kipindi hiki cha mpito wakati wakisubiri maelekezo kutoka LATRA wameomba nauli zibaku zile walizipandisha kwani ni rafiki kulingana na bei ya mafuta ya sasa, hivyo hawapingani na maagizo ya serikali licha ya kuwataka kutopndisha nauli,” amesema mmoja wa madereva hao.
Aidha, madereva hao walisema kama maombi yao hayatatekelezwa kupanda kwa nauli watasitisha safari za kutoka Itumba hadi Mpemba Bali watakuwa wanaanzia Isongole hadi Mpemba kwa nauli ya Sh 1,900, kwani kutoka Isongole mpaka Itumba hawatozi nauli.
Hivi karibuni Afisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri(LATRA), Christiano Lupala mkoani Songwe alisema hakuna mabadiliko ya nauli hivi sasa na mabadiliko hayafanyiki kiholela na atakayebainika kukiuka kanuni na taratibu atawajibishwa kwa mujibu wa Sheria.