26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

DC ILALA AWAONYA MADIWANI

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amewaonya madiwani na watendaji wa Manispaa ya Ilala kuacha kutumia madaraka yao vibaya kwa kuingiza biashara zao kinyemela katika zabuni mbalimbali zinazotolewa kwa maslahi ya jamii.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa madiwani yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili, Sophia alisema ili utawala uweze kuhesabiwa kuwa ni bora, kunahitajika misingi imara ya kuzingatia sheria ya maadili.

Alisema ni mwiko kwa diwani au kiongozi yeyote kuingiza biashara zake katika shughuli za kijamii kwa lengo la kujipatia kipato na anayefanya hivyo anakiuka maadili na hafai kuwa kiongozi.

“Baraza hili ndilo lenye majukumu mazito, mnalazimika kuzingatia misingi ya maadili, kwa kuwa moja ya wajibu mkubwa wa viongozi wa umma ni kukuza na kusimamia maadili, hivyo uadilifu ni zaidi ya kuzingatia sheria, taratibu na kanuni kwa sababu wahusika wa kupitisha tenda katika manispaa ni nyinyi, jaribuni kuwa makini na mjiepushe kujiingiza kwa lengo la kupata cha juu,” alisema Sophia.

Alisema moja ya misingi ya demokrasia ni kuwa na Serikali inayowajibika kwa wananchi na yenye viongozi wanaowatumikia wananchi kwa uadilifu, hivyo kiongozi yeyote au aliyeajiriwa na Serikali anatakiwa atumie wadhifa wake kwa manufaa ya wananchi na si yake binafsi.

Pia alisema uadilifu ni sharti ujengwe ndani ya jamii, ili uwe sehemu ya utamaduni wa nchi na utekelezaji wa maadili unahitajika ushirikiano baina ya viongozi, wananchi na wadau mbalimbali.

Aliwataka madiwani hao kuwa wawazi wakati wote, ikiwa ni pamoja na kutangaza mali pamoja na idadi ya familia zao wanazozihudumia ili kutekeleza sheria hiyo.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wana sifa za kujinufaisha wenyewe, jambo lisilostahili na ni kinyume na sheria za maadili.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili, Evodia Pangani, alisema sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya 1995 na marekebisho yake inahusu mgongano wa maslahi, tamko la rasilimali na madeni na utekelezaji wa ahadi na uadilifu.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia watendaji hao kujifunza misingi ya maadili, umuhimu wake na athari za kukosa maadili.

Naye Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, alisema ni vyema madiwani wakazingatia mafunzo hayo kwa sababu maadili yanaanzia ngazi ya kaya.

Alisema jamii isiyo na maadili haina maendeleo, kwa sababu hakutakuwa na usikivu na badala yake kutajengeka kizazi kisicho na faida na maendeleo kwa jamii.

“Mafunzo haya yatasaidia kujifunza kwa undani utekelezaji wa sheria ya maadili, ikiwa ni pamoja na kupiga vita ukiukwaji wa maadili,” alisema Kuyeko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles