31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DC Hanang ageuka mbogo kwa Polisi

Mohamed Hamad, Kiteto

Mkuu wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Joseph Mkirikiti ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kushughulikia matukio 11 ya ukatili yanayosababisha madhara kwa jamii.

Mkiriti ameyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) wakishirikiana na Shirika la Msaada wa Sheria kwa wanawake (WLAC) wanaotekeleza mradi huo chini ya Ufadhili wa Foundation For Civil Society kuwa wanakusudia kufikia wananchi 27,000.

Ameyataja matukio hayo ni kutoroshwa binti wa miaka 12 aliyekuwa anasoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Bastuqah, Kata ya Hidet, ubakaji na ulawiti, hatma ya mtoto aliyekataa shule Kata ya Bassoutu na hatma ya mtoto wa miaka mitatu aliyetekwa Kijiji cha Masakta.

“Walimu kuripotiwa kufanya mapenzi na wanafunzi, kubaka na kuwapachika mimba wanafunzi, baadhi ya jamii kushabikia vitendo vya kikatili na kushindwa kulinda haki ya mtoto na malalamiko ya kupotea kwa haki ya mirathi vyombo vya sheria, haya yote nataka myashughulikie,” alisema.

Alisema matukio mengine ni watuhumiwa wa ubakaji kupewa ushirikiano na polisi kisha kutolewa na kuendeleza uhasama kwa jamii kutoa vitisho na majigambo hivyo kufanya wananchi kutokuwa na imani na vyombo vyao vya dola.

Awali, akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Hanang (HALISO), Dominick Duncan, katika mafunzo hayo wanatoa elimu ya sheria na machapisho mbalimbali ya kisheria wilayani humo, kwa lengo la kufanya wananchi kuwa na msingi wa sheria ili kujenga jamii inayoheshimu utawala wa sheria, utawala bora, kulinda na kutekeleza misingi ya haki za binadamu.

Alitaja maeneo yatakayofikiwa na mradi huo kuwa ni Kata za Katesh, Ganana, Gehandu, Bassotu, Mulbadaw, Dirma, Gendabi, Endasaki, Simbay, Sirop, Dumbeta, Jorodom, Mogitu, Balangdalalu, Lalaji na Nangwa.

Kwa upande wake Mratibu wa Uwezeshaji jamii Kisheria, kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria wa Wanawake na Watoto (WLAC), Consolata Chikoti alisema, Wilaya ya Hanang ina asilimia 58 za Ukeketaji tofauti na maeneo mengine nchini kutokana na mila na tamaduni za wenyeji wa eneo hilo.

“Takwimu ya mwaka 2015-2016 kuhusu ukeketaji zinaonyesha Mkoa wa Manyara unaongoza kwa asilimia 58, huku vitendo vingine vya ukatili vikiendelea kama vile mimba za utotoni, vipigo, ubakaji, utakaso wa wajane na ndoa za utotoni,” alisema Chikoti

Alisema serikali kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili imeanzisha mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto ujulikanao kwa jina la (MTAKUWWA) utakaotekelezwa mwaka 2017/18, 2018/19 na 2020/21 na kuanzisha kamati za mpango huo katika kila ngazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles