33.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

DC awataka wamiliki wa viwanda kuzingatia miongozo ya OSHA

Na Mwandishi Wetu, Pwani

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filbert Sanga, ametoa wito kwa wamiliki wa maeneo ya kazi hususan viwanda katika Wilayani ya Mkuranga Mkoani Pwani kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ili Mamlaka hiyo iweze kuwaongoza katika kuboresha mazingira yao ya kazi.

Sanga ameyasema hayo  ofisini kwake alipotembelewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ambaye alifanya ziara katika Kiwanda cha Fujian Hexingwang kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya kuboresha mifumo ya usalama na afya katika kiwanda hicho yaliyotolewa awali na wataalam kutoka OSHA.

“Nawashukuru OSHA kutembelea kiwanda chetu cha Fujian Hexingwang kinachozalisha nondo na kuchukua hatua kufuatia ajali iliyotokea mwezi uliopita. Naomba ziara hizi ziendelee pia kwenye viwanda vyote vilivyopo wilayani kwetu ili kuhakikisha kwamba wamiliki wa viwanda wanafuata na kutekeleza maelekezo yote yanayohusu uboreshaji wa usalama na afya kwa wafanyakazi,” aliosema Sanga.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiongea baada ya kukagua maboresho yaliyofanyika katika kiwanda hicho, amesema Taasisi yake imeridhishwa na maboresho ya awali yaliyofanyika na hivyo kuondoa hati ya zuio la kufanya uzalishaji iliyotolewa hapo awali ambapo wametoa hati ya maboresho (improvement notice).

 “Tumejionea maboresho mengi ambayo kiwanda hiki kimejitahidi kuyafanya ikiwemo kufunga mashine (Feeder scooper trolley) ambazo zitasaidia kazi zilizokuwa zinafanywa na wafanyakazi, sasa kazi hizo zitafanywa na mashine na hivyo kupunguza hatari ya ajali kwenye eneo hilo, alifafanua Mwenda na kuongeza:

“Agizo lingine ambalo tunaona utekelezaji wake umefanyika ni pamoja na kuweka mtaalamu wa utambuzi wa vyuma ambavyo vinaweza kusababisha milipuko. Hii itasaidia sana kuhakikisha vyuma vinavyoenda kwenye moto ili kuzalisha uji ambao unatengeneza nondo ni vile tu ambavyo vinastahili kuchomwa. Aidha, wamefanya maboresho katika utoaji wa vifaa kinga stahiki kwa wafanyakazi.”

Kufuatia maboresho hayo, Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA, amesema wameoandoa hati ya zuio walilolitoa katika kiwanda hicho baada ya kusababisha ajali na kuwapatia hati ya maboresho (improvement notice).

Aidha,  ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuendelea kuboresha zaidi eneo lao la kazi na kuhakisha wanawasiliana na mamlaka  nyingine za serikali ambazo zilipita kwenye kiwanda hicho, kuangalia utekelezaji wa maboresho yaliyofanyika ili kiwanda hicho kiendelee na uzalishaji.

Meneja wa Kiwanda cha Fujian Hexingwang, XU XINGDA, ameishukuru OSHA kwa ushirikiano na maelekezo ambayo wamekuwa wakiyatoa katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa kiwanda hicho wanafanya kazi katika mazingira salama.

Kwa upande wao wafanyakazi wa kiwanda hicho, wameishukuru OSHA na uongozi wa kiwanda chao kwa jitihada ambazo wamezifanya katika kuhakikisha kiwanda hicho kinaboresha mazingira ya kufanyia kazi.

Mwezi uliopita, ajali ilitokea katika kiwanda cha Fujian Hexing wang kutokana na mlipuko katika majiko ya kuyeyushia vyuma chakavu na kupelekea vifo vya wafanyakazi wawili. Kufuatia ajali hiyo, OSHA ilifanya uchunguzi wa ajali na kubaina chanzo chake na hivyo kuelekeza kiwanda hicho kufanya maboresho katika mifumo yake ya usalama na afya mahali pa kazi.

Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani ni miongoni mwa Wilaya zenye viwanda vingi katika mkoa wa Pwani ambapo inakadiriwa kuwa na viwanda vipatavyo 130.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,882FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles