DC AWAONYA WANAOTUMIA MIZANI FEKI KWA WAVUVI

0
567

 

Na SAMWEL MWANGA


MKUU wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera ameagiza kukamatwa kwa wafanyabiashara wanaotumia mizani  bandia katika shughuli  za uvuvi kando ya Ziwa Victoria na kuwaibia wauzaji wa samaki.

Mwera alimuagiza Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoani Simiyu kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafanyabiashara wazaotumia mizani mbovu ambazo zimeshapigwa marufuku na serikali.

Alisema  watu wote wanaojishughulisha na kazi za kuuza na kununua samaki wanapaswa kutambua kuwa ndani ya wilaya hiyo hakuna mwananchi yeyote kunyanyaswa kwa namna moja au nyingine.

“Katika Wilaya ya Busega sitakubali kuona mwananchi yeyote hasa wale wa kipato cha chini  kunyanyaswa na huku anafanya kazi yake ambayo ni halali na yenye manufaa kwake.

“Aliagiza jeshi la polisi kwa kushirikiana na Wakala wa Mizani (WMA) kuanzia msako mkali kila siku katika maeneo ya kando ya Ziwa Victoria ndani ya Wilaya ya Busega kuzihakiki mizani zote zinazotumika kupimia samaki kama iko salama.

“Nimetoa siku saba kwa wanunuzi wote wa samaki wilayani Busega  waweze kusalimisha mizani feki katika ofisi za watendaji wa vijiji  iweze kufanyiwa uhakiki  na kuwekewa nembo inayotambulika na serikali,” alisema.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali kwa wale ambao watakaokuwa wanatumia ujanja wa kuficha mizani wakati wa ukaguzi na   kuitoa mara baadaye   waweze kuchukuliwa hatua kali za  sheria juu yao.

Alisema   mizani ambayo ni feki ni wizi wa hali ya juu kwa serikali na wachuuzi wadogo kwa vile  wanawapunja kwa kuwaibia  hivyo ni lazima mizani iwe laini kama inavyokuwa inatoka madukani.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Simiyu, Augustino Amoni aliwataka wafanyabiashara wote   kujitokeza  haraka ili kufanikisha hatua hiyo kabla ya kumalizika  siku saba zilizotolewa na mkuu wa wilaya.

Alisema  watu wengi wamekuwa wakipima kienyeji bidhaa zao kwa kutumia mabakuli, ndoo na vitu vingine huku wakijua hicho ni kinyume na taratibu za vipimo.

“Tutaweka  kambi katika Wilaya ya Busega tuwe tunafanya uchunguzi wa mara kwa mara   wa mizani zote  maeneo ya kandokando ya ziwa Victoria   kuwasaidia wananchi wanaoibiwa na wafanyabiashara kwa kutumia mizani feki,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here