Florence Sanawa, Newala
Mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo amewaonya wakazi wa Kijiji cha Mitema halmashauri ya wilaya ya Newala kuacha mara moja kutumia vibaya chanzo hicho kwa shughuli hatarishi ikiwemo matambiko.
Akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa uhifadhi wa chanzo hicho amesema kuwa shughuli hatarishi Katika vyanzo vya maji zimekuwa zikiharibu na kuchafua vyanzo hivyo ambavyo zaidi ya wakazi laki tano wa wilaya mbili za Tandahimba, Newala na Halmashauri ya Mji Nanyamba wanategemea kupata huduma ya maji.
Amesema kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia makatazo ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi ili kulinda na kutunza vyanzo hivyo ambavyo vimekuwa vikisaidia wananchi kupata huduma za maji ambazo ni muhimu kwa maisha ya binadamu.
“Unajua Miaka ya nyuma wananchi wa chanzo hiki walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kibinadamu hali ambazo zilikuwa zikiharibu na kuhatarisha maisha lakini baada ya elimu kutolewa usimamizi umekuwa mzuri na eneo kubwa limekuwa likilindwa bila kuwepo kwa hatari yoyote.
“Kumekuwa na vyanzo vingine ikiwemo mkunya vimekuwa vikichafuliwa na wananchi kwa matumizi yasiyofaa ikiwemo kufanya matambiko kwa kujisaidia na kuchinja wanyama, ukataji wa miti hovyo hii sio sawa lazima tukemee na tushirikiane ili kulinda na kutunza vyanzo vya maji vinavyotusaidia katika upatikanaji wa huduma hiyo,” amesema Mangosongo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini, Sudi Mpemba amesema wameweka mikakati kabambe kuhakikisha kuwa kwa mwaka wanaweza kuhifadhi vyanzo 10 vya maji kwa kuvipa kipaumbele chanzo cha mitema kwakuwa kina uwezo mkubwa wa kuzalisha maji pia kinahudumia wakazi zaidi ya laki tano.