25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

DC aongoza kampeni ulipaji kodi pango la ardhi

Mwandishi Wetu -Shinyanga

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ameongoza kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya Pango la Ardhi kwa wamiliki wa viwanja vya biashara na makazi katika manispaa ya Shinyanga inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kutoa elimu ya ulipaji kodi na kufuatilia wadaiwa wenye madeni makubwa na malimbikizo ya muda mrefu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mjini hapa, DC Mboneko,  alisema ni wajibu wa kila mmiliki wa ardhi kuhakikisha analipia kodi ya pango la ardhi hata kama hana hati ya ardhi akibainisha kuwa kutolipa kodi ya pango la ardhi ni kuiibia serikali hivyo kuchangia kudhorotesha maendeleo ya nchi.

“Msiidanganye serikali kwa sababu serikali ina macho makubwa, ina macho marefu itawafuata popote mlipo ili mlipe kodi. Ni lazima deni lilipwe, tutahakikisha tunawafuatilia wale wote wanaodaiwa kwani kodi zinazokusanywa ndiyo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

 “Niwashukuru na kuwapongeza wafanyabiashara na wananchi tuliowafikia leo mmeonesha kutambua umuhimu wa kulipa kodi ya pango la ardhi na mmesema mpo tayari kulipa madeni yenu. Hakikisheni mnalipa madeni yenu kabla ya mwaka wa fedha haujaisha Juni, 2020. Tutaendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili kuhakikisha kila mmoja analipa kodi ya ardhi anayodaiwa,” alisema Mboneko.

Kwa upande wao wafanyabiashara na wananchi wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi wameishukuru serikali kuwatembelea na kuwakumbusha wajibu wao kulipa kodi huku wakibainisha kuwa wapo tayari kulipa madeni yao.

“Mimi sikujua kuwa ukiwa na kiwanja tu bila hati ya ardhi unatakiwa ulipie kodi ya pango la ardhi.Nilijua nikipata hati ndiyo naanza kulipia. Nimejipanga kuanza kulipa deni ninalodaiwa ambapo hadi mwisho mwezi huu wa Aprili nitakuwa nimemaliza kulipa deni,” alisema Polycarp Kimario ambaye ni Mkurugenzi wa Mwananchi Garage.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha Fang’ Wah, Alice Mingyang Yan,  alisema wapo tayari kulipa deni lao wanalodaiwa kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2020 muda ambao wamekuwa wakifanya shughuli zao badala ya kudaiwa kuanzia mwaka 2013 kipindi ambacho kulikuwa na wawekezaji wengine waliouza kiwanja.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo alisema anatambua umuhimu wa kulipa kodi na tayari alishaanza kulipa deni analodaiwa akibainisha kuwa awali alikuwa anadaiwa Sh milioni 30 lakini deni lake limekuwa likiongezeka kutokana na mgogoro wa ardhi uliokuwepo katika kiwanja chake kilichopo eneo la Matanda.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami alisema lengo la kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kwa wamiliki wa viwanja vya Biashara na makazi inayoendeshwa katika mikoa mbalimbali ni kutoa elimu ya ulipaji kodi ya pango la ardhi na kufuatilia wadaiwa wenye madeni makubwa na malimbikizo ya muda mrefu.

“Kampeni hii pia inalenga kutatua changamoto zinazowakabili walipa kodi na kuchukua hatua za kisheria kwa kusambaza hati za madai ili kuwafikisha mahakamani watakaokaidi tutawakamata mali na kuuza ili kufidia deni husika,” alisema Masami.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles