Derick Milton, Bariadi
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga amemtwisha mzigo wa lawana Ofisa Afya wa halmashauri hiyo kwa kushindwa kuwajibika kutokana mji huo ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Simiyu kukithiri kwa uchafu.
Mbali na hilo, Kiswaga amemtupia lawama Katibu Tarafa ya Bariadi, watendaji wa kata, kwa kile alichosema kuwa wao ndiyo sababu ya mji huo kukithiri kwa uchafu.
Kiswaga amesema hayo leo Alhamisi Januari 9, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, kilichofanyika katika ukumbi wa Bardeco Mjini hapa.
Amesema wanaotakiwa kubeba mzigo wa lawama ni watendaji hao, ambao wameshindwa kuwasimamia wananchi kuhakikisha mji unakuwa safi kama inavyotakiwa.
“Hatuwezi kuwa na mji ambao serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 20 halafu ni mchafu, Ofisa Afya na usafi wa mazingira na katibu tarafa lazima wajitafakari katika hili, kama hawawezi kuna sehemu nyingine za kufanya kazi.
“Kila sehemu ni uchafu, mitaro yote michafu, imefikia hatua Mimi mwenyewe naingia mtaani kusimamia wananchi wafanye usafi wakati wahusika wapo, sasa nitoe onyo sitaweza kufanya kazi na watu ambao hawawezi kuwajibika,” amesema Kiswaga.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka watumishi hao kwa kushirikiana na watendaji wa mitaa na kata kuhakikisha wanasimamia suala la afya, huku akiwataka madiwani kutoingilia suala hilo.