SAM BAHARI – SHINYANGA.
WADAU wa elimu Mkoa wa Shinyanga wamekemea tabia ya wanafunzi wa kike wanaosoma shule za msingi na sekondari kuwatongoza wavulana kwa lugha ya kuvutia na yenye kushawishi kushiriki vitendo vya mapenzi.
Licha ya kuibuka tabia hiyo, wadau wameiomba Serikali kupitia upya sheria inayosimamia wanafunzi wa kike wanaopewa mimba na kukatisha masomo yao.
Akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza matokeo ya darasa la saba juzi, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba alisema imebainika wanafunzi wa kike kipindi hiki wameanza kuwatongoza wavulana na kufanya ngono isiyo salama na mwisho wa siku hupata ujauzito.
Alisema wasichana kuamua kubadilika tabia na kuanza kuwatongoza wavulani, ni kutokana na ulegevu wa sheria inayotumika kwa watu wanaowapa mimba hukamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani tofauti na mtoto wa kike ambaye hubaki huru.
“Sheria hii inayohusu wanafunzi wetu wa kike kupewa mimba, inatafasiri mwanaume aliyempa mimba mwanafunzi akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili, lakini mtoto wa kike anayetiwa mimba hubaki huru,” alisema.
Akitangaza ufaulu wa matokeo ya mitihani wa darasa la saba, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albart Msovela alisema kwa mara ya kwanza mkoa huo umeshika nafasi ya 17 kitaifa.
Alisema mkoa uliandikisha watoto 40,292 kuanza darasa la kwanza mwaka 2013 na waliosajiliwa kufanya mtihani wa mwisho kuingia kidato cha kwanza mwaka 2020, ni 30,393 na waliofaulu ni 23,634 sawa na asilimia 77. 76.