26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

DC ahimiza wazazi kuzingatia malezi ya watoto

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

WAZAZI na walezi wametakiwa kutenga muda wa kukaa na watoto na kuzungumza nao ili kutambua changamoto wanazokutana nazo ikiwemo ukatili wa kijinsia, pia kubaini mienendo yao.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Edward Balele, alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta, katika uzinduzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Vuka Initiative.

Balele alisema kwa sasa asilimia kubwa ya jamii imejisahau katika malezi ya watoto ambapo muda mwingi wamekuwa wakiutumia katika shughuli za kiuchumi na kusahau majukumu ya kifamilia.

Alisema ni muhimu wazazi na walezi kutenga muda maalum wa kuzungumza na watoto ili waweze kubaini wanayokumbana nayo kuanzia mazingira ya shule hadi majumbani.

“Kwa kufanya hivyo itawasaidia kutambua baadhi ya changamoto ikiwemo za ukatili wa kijinsia ambao unakabili watoto wengi,huku wengine wakiathirika na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa bila wazazi kujua,” alisema.

Mkuu huyo aliipongeza taasisi hiyo kwa kuungana na serikali na wadau wengine katika kuhamasisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake, wasichana na watoto.

“Nawapongeza kwa kuja na kampeni hii ya “Mwogeshe mwanao”,imekuja kwa wakati sahihi kwani jamii imejisahau kwa kiasi kikubwa katika malezi ya watoto,” alisema.

Alisema kampeni hiyo ni muhimu na itasaidia kupunguza changamoto za ukatili wa kijinsia hususani katika jamii za kifugaji.

Awali, Mkurugenzi na mwanzilishi wa taasisi hiyo, Veronica Ignatus, alisema wanajishughulisha na  utoaji wa elimu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.

Alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine pamoja na serikali wameanza kuelimisha makundi mbalimbali ikiwemo wanawake na watoto, ili waweze kutambua aina za ukatili na umuhimu wa kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya kikatili.

Akizungumza Kampeni ya “Mwogeshe mwanao”, alisema imelenga kuwakumbusha wazazi na walezi kuhusu jukumu la kuzingatia malezi bora na kuwa wafuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya watoto wao.

“Tumebaini moja ya visababishi vya ukatili wa kijinsia kwa watoto ni pamoja na wazazi na walezi kutokuwa na ukaribu na watoto wao huku baadhi ya mila na desturi potofu zikichangia ukatili wa kijinsia,” alisema Veronica

Alisema kwa kuanzia wanatarajia kufikia makundi mengine ikiwemo wafanyakazi wa sekta rasmi na zisizo rasmi ikiwemo mamalishe, wajasiriamali mbalimbali kutoka wilaya za Arumeru, Arusha, Karatu, Longido na Ngorongoro.

“Tumebaini watoto wengi huathirika kwa kupigwa na kutendewa vitendo vya kikatili kuanzia na watu wa karibu kama ndugu,jamaa au wazazi pamoja na shuleni,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,734FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles