28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dawasa yakabidhiwa mradi wa maji Same – Mwanga – Korogwe

Na Mwandishi Wetu, Same

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepewa kazi ya kukamilisha mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe baada ya Mkandarasi wa awali Kampuni za M. A Kharafi & Sons na BADR East African Enterprises Ltd kusitishiwa mkataba Desemba 2020.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya mradi huo iliyofanyika wilayani Mwanga, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali itasimamia haki na madai ya waliokuwa wafanyakazi wa kampuni hizo na haitamvumilia mkandarasi mzembe au mtaalam atakayechelewesha mradi wa maji kukamilika kwa wakati.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa uendelezaji mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe.

Amesema baadhi ya kazi kama ufungaji mifumo na mitambo ya umeme zitafanywa na wakandarasi na utaratibu wa kuwapatia umeshaanza ili kila jambo lifanyike kwa wakati na kukamilika.

Aidha amewataka wataalam wa manunuzi kuhakikisha watoa huduma na wakandarasi wanaopatikana wanakuwa bora ili kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kama ilivyopangwa.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, amesema Serikali na wataalam wake wamepanga kuchukua miradi yote ambayo wakandarasi watalegalega.

Pia ametoa onyo kwa wakandarasi wanaozidisha gharama za miradi kwa sababu watapoteza sifa za kutekeleza miradi hiyo.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyrpian Luhemeja, amewahakikishia viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa kazi ya kukamilisha mradi huo wanaimudu na kuahidi itakamilika ifikapo Desemba 2021.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akiwasha mashine ya kuunganisha mabomba wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe kwa Dawasa.

Mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe utakaozalisha zaidi ya lita milioni 65 kwa siku utakuwa na tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 19 ambalo litakuwa kubwa kuliko matanki yote mkoani Kilimanjaro na utahusisha ulazaji mabomba yenye urefu wa kilomita 265.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akipata maelezo kuhusu maeneo yatakayohudumiwa na mradi.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles