27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Dawasa wapewa siku 14 kupitia mifumo majitaka Buguruni

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, ametoa siku 14 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) kupitia mifumo ya majitaka katika Kata ya Buguruni kubaini ambayo inapeleka maji katika mfereji wa kupokea maji ya mvua.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Mivinjeni baada ya kukagua mfereji unaopokea maji ya mvua.

Mfereji huo wenye urefu wa kilomita moja unajengwa katika Mtaa wa Mivinjeni Kata ya Buguruni unagharimu Sh bilioni 3.2 lakini baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wameanza kuelekeza mabomba ya majitaka.

Akizungumza baada ya kufanya ziara katika eneo hilo Ludigija amesema mradi huo uko kwenye hatua za mwisho kukamilika na kuagiza mifumo yote ya majitaka inayoingia kwenye mfereji huo iondolewe mara moja.

“Tunajenga miradi hii kwa manufaa ya kukusanya maji ya mvua lakini wengine wanaweka majitaka matokeo yake mvua zinapoanza kunyesha tunaweza kukutana na mlipuko wa magonjwa tusiyotarajia. Lengo la miradi hii ni kuwakomboa wananchi kwa kuwapunguzia adha ya mafuriko na kuhakikisha afya zao zinalindwa,” amesema Ludigija. 

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mivinjeni, Fadiga Legele, amesema wananchi wamekuwa wakikumbana na adha ya kukanyaga majitaka kutokana na utiririshwaji wa vinyesi uliokithiri.

“Miaka iliyopita wananchi waliunganisha mifumo yao ya majitaka kwenye mfereji huu lakini sheria ya mazingira na kupitia miradi ya DMDP inatukataza lakini maeneo mengi yana changamoto ya chemchem, tunapochimba makaro yanakuwa hayafiki kina kirefu utakuta vinyesi vinatiririka wananchi kila siku wanatuvamia viongozi na haya mambo yako nje ya uwezo wetu,” amesema Legele.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi Dawasa, Ramadhani Mtindasi, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya mkuu wa wilaya na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwenye nyumba ambazo zimeunganishwa kwenye bomba la maji ya mvua.

Amesema pia wanatarajia kujenga miradi miwili katika eneo hilo kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ukiwemo mtambo mkubwa wa kuchakata majitaka na ule wa kutoa majitaka kwa kutumia mfumo rahisi na kwamba wako kwenye hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Katika hatua nyingine Wilaya ya Ilala imezindua zoezi la uwekaji anwani za makazi na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vijana watakaokuwa wakifanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles