23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Dawasa inavyopambana kusambaza maji Dar, Pwani

CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

MAJI ni uhai na huduma muhimu kwa maisha ya binadamu yeyote, endapo  itakosekana huchangia kuenea kwa magonjwa ya mlipuko na vifo.

Machi 22 kila mwaka ni kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, ambapo Jiji la Dar es Salaam litaungana na Watanzania wengine kusherehekea.

Kauli mbiu ya wiki ya maji kwa mwaka huu ni; ‘Usimwache mtu nyuma katika kupata huduma ya maji.’

Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) imeongeza jitihada za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi hasa waliokuwa pembezoni.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja, anaeleza kuhusu jitihada za mamlaka hiyo katika kuenzi na kutekeleza miradi na kufikia wananchi ambao awali walikuwa hawana huduma.

Maelezo ya Luhemeja yanakwenda sambamba na kauli mbiu ya wiki ya maji mwaka huu.

Anasema Dawasa imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali itakayowafikia wananchi waliokuwa hawapati huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.

Anasema miradi hiyo iliyoanza kutekelezwa hivi karibuni ni mpango mkakati wa kuwafikia Watanzania wengi zaidi waishio Dar es Salaam na katika miji ya Mkoa wa Pwani ambapo DAWASA inatoa huduma.

Anasema miradi hiyo imeanza kuzaa matunda baada ya wakazi wa maeneo ambayo hayakuwa na huduma ya upatikanaji wa maji sasa yanapata.

“Mfano ni eneo la Salasala na Kinzudi ambalo halikuwa na maji kabisa lakini sasa linapata maji baada ya mradi kukamilika kwa ulazaji wa bomba kwa km 48 na ujenzi wa tenki kubwa la ujazo wa lita 6,000,000 eneo hilo pamoja na kituo cha kusukuma maji (Booster station),” anasema Mhandisi Luhemeja.

Anaongeza kuwa  katika mradi huo zaidi ya wakazi 5,400 wameunganishiwa huduma huku akitoa wito kwa wananchi ambao wanahitaji huduma ya kuunganishiwa wajitokeze na kupatiwa.

Akizungumzia mradi mwingine ambao sasa wananchi wanapata maji, Luhemeja anasema ni ule wa eneo la Kiembeni Bagamoyo mkoani Pwani, ambalo halikuwa na maji kabla ya mradi wa maji maarufu wa Kiembeni kuanza kutoa huduma.

Anasema baada ya kukamilika, wananchi zaidi ya 2,000 wameunganishwa na kuanza kupata huduma ya maji safi na salama.

Anaongeza kuwa mradi mwingine ni wa 2D uliotekelezwa eneo la Kiluvya, Kibamba, Hondogo, Mloganzila na Kwembe.

“Mradi huu nao umekamilika na wananchi wa maeneo haya wataanza kunufaika na huduma ya maji kwa awamu, kadiri maunganisho ya maji yanavyoendelea kufanyika ambapo hadi sasa takribani wananchi 6,500 wameshapatiwa huduma,” anasema.

Anasema katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa Kiwalani Bombom na vitongoji vingine, Dawasa imekamilisha mradi wa maji katika eneo hilo.

“Mradi huu wa awamu mbili umekamilika na wananchi takriban 700 wameunganishwa na kupata huduma kutoka katika mradi huu,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Aidha, anasema bado kuna miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Dawasa ili kuhakikisha hakuna mkazi wa eneo lake la huduma anakosa maji.

Anasema moja ya miradi ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilishwa ni ule wa Bonyokwa ambao mara baada ya kukamilika wananchi wataanza kuunganishiwa maji.

“Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kuwahudumia wakazi 30,000 wa kata ya Bonyokwa na maeneo ya jirani,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Anasema miradi yote hiyo inayotekeleza kwa fedha za ndani itakwenda kutatua changamoto za maji katika maeneo mbalimbali ya jiji hili na hivyo kwenda sambamba na kaulimbiu ya mwaka huu.

 “Kaulimbiu ya wiki ya maji mwaka huu inatutaka kutokumwacha mtu katika utoaji wa huduma ya maji hivyo nasi tumejipanga kuhakikisha kila mkazi wa Dar es Salaam na miji ya Bagamoyo, Pwani na Mkuranga wanapata maji,” anasema.

Naye Meneja wa Utekelezaji Miradi ya Maji, Mhandisi Ramadhani Mtindasi, anasema katika Kata ya Kisukuru, Manispaa ya Ilala, Dawasa ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mradi.

“Tunapeleka maji katika Kata ya Kisukuru ambapo utekelezaji unaendelea na lengo ni kuhudumia wakazi zaidi ya 15,000,” anasema Mtindasi

Anasema katika Manispaa ya Ubungo, kuna mradi wa maji ambao utawahudumia wakazi wa Saranga na vitongoji unaoendelea kwa sasa.

Anaongeza kuwa utakapokamilika mradi huo unategemewa kuwahudumia wakazi wa kata hiyo wasiopungua 15,000.

Mtindasi anasema pia eneo la Kwa Mtoro kuna mradi unaoendelea ukiwa katika hatua za mwisho ambao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

“Mradi huu utaenda kujibu na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo la Kimara kwa Mtoro na vitongoji vyake na tunategemea utahudumia wateja wasiopungua 10,000,” anasema Mtindasi.

Akizungumzia kuhusu miradi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni, anasema mmoja wake ni ule wa mji wa Mkuranga.

“Tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi na hivi karibuni tutaanza ujenzi wa mradi huu ambao kama ukikamilika utahudumia wakazi 25,000 wa Mkuranga na vitongoji vyake,” anasema.

Mtindasi anasema mamlaka hiyo ipo  katika hatua za manunuzi ili kutekeleza mradi wa maji wa visima vya Kimbiji. 

“Wakazi wa Manispaa ya Kigamboni wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na ya uhakika kupitia visima vya Kimbiji, unategemea kujibu sehemu kubwa ya changamoto za maji katika eneo hilo,” anasema.

 Akizungumzia kuhusu Dar es Salaam ya Kusini ambayo imekuwa haina mtandao wa maji ya bomba kwa muda mrefu, Mtindasi anasema kuna mradi wa maji unaotekelezwa katika eneo la Jet Buza.

“Mradi huu utawanufaisha wakazi wa Dar es Salaam ya Kusini ikiwa ni pamoja na Buza, Yombo, Mwanagati, pamoja na Mbagala,” anasema.

Anasema Dawasa imeongeza mradi mwingine wa maji katika eneo la Kiwalani huku mingine miwili ambayo ni wa awamu ya kwanza na pili ikiendelea kutekelezwa.

“Mradi wa Kiwalani awamu ya tatu upo kwenye utekelezaji na lengo lake ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji na kuendeleza mradi ulioanza wa Kiwalani awamu ya kwanza na ya pili,” anasema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Neli Msuya, anawataka wakazi wa Dar es Salaam kuwaunga mkono kwa kuhakikisha wanalipa ankara zao kwa wakati ili kuwezesha huduma hiyo kuwafikia watu wengi zaidi.

“Niwaombe wakazi wa Dar es Salaam na mkoa wa Pwani kuhakikisha wanalinda miundombinu ya maji na kulinda vyanzo vya maji ili huduma iwe endelevu,” anasema Neli.

Hivi karibuni Dawasa na iliyokuwa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(Dawasco) ziliunganishwa ili kuwa na mamlaka yenye nguvu ambapo kazi za ujenzi wa miundombinu na usambazaji  maji zinafanywa nayo.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles