28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Dawa za kutibu maradhi zinazopunguza nguvu za kiume

wanandoaNa Hamisa Maganga, Dar es Salaam

ZAMANI, tatizo la nguvu za kiume kwa asilimia kubwa lilikuwa likiwapata wazee. Hili lilikuwa ni jambo la kawaida kwa watu wenye umri mkubwa. Kwa kiasi kikubwa hali hii ilitokana kwamba watu waliofikia umri huu huwa wanakabiliwa na maradhi mengi ikiwamo sukari na shinikizo la damu.

Hata hivyo, kwa kawaida binadamu hastahili kuzeeka na magonjwa, lakini hali hii hutokea kutokana na mfumo wa maisha waliojiwekea. Watu wanaishi maisha ya kifahari na kusahau kuzingatia suala la afya.

Tofauti na zamani, siku hizi watu wanaokabiliwa na tatizo la nguvu za kiume ni vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30.

 

SABABU ZA KUPUNGUA NGUVU ZA KIUME

 Boaz Mkumbo, ni daktari mwelimishaji wa magonjwa ya lishe, kitambi, uzito mkubwa, kisukari, saratani, vidonda vya tumbo na kiungulia sugu, anasema katika mwili wa binadamu kuna vichocheo aina ya ‘testosterone’ ambavyo hutolewa kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa ubongo, ufanye kazi katika hali tulivu, kuondoa msongo, mstuko wa aina yoyote, kuimarisha uwezo wa kufikiri, kuimarisha furaha ya mwili na nguvu za kiume.

Anasema endapo kichecheo hiki kikivurugika, kinasababisha vichocheo vingine kama insulin, leptin, cortisol na vichocheo vya ukuaji pia kuvurugika na matokeo ya hitililafu hii mwilini ni kupungukiwa kwa nguvu za kiume.

Anasema vichocheo hivi hufanya kazi kwa ushirikiano hivyo, endapo kimoja wapo kitavurugika, vyote vinapoteza mwelekeo hatimaye tatizo kuwa sugu zaidi.

 

TESTOSTERONE

Dk. Mkumbo anasema kuwa kichocheo hiki ndio silaha ya mwanamume kwa kuwa humfanya kuwa imara katika tendo la ndoa. Upungufu wa kichocheo hiki husababisha kukosa matamanio kwa jinsia tofauti, kupungua kwa nguvu za misuli kiutendaji, mafuta kurundikana ovyo mwilini (Belly fat and Obesity).

“Kichocheo hiki hakipatikani kwa wanaume tu, bali hata kwa wanawake ingawa ni kwa kiwango cha chini mno.

“Endapo kikipungua kinaweza kumsababishia mwanamke kukosa matamanio wakati wa tendo la ndoa au misuli kushindwa kuhimili tendo la ndoa (kuchoka), kuongezeka uzito kupita kiasi na nyama uzembe, pia kupunguza uwezo wa kufikiri na kumbukumbu,” anasema Dk. Mkumbo.

Aidha, anataja baadhi ya vitu vinavyochangia kupunguza nguvu za kiume kuwa ni vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda.

Anasema kuwa kiwango kimoja cha kichecheo kikivurugika vyote vinavurugika hivyo, inatakiwa kulinda kiwango cha insulin kuwa katika hali nzuri muda wote ili kufurahia tendo la ndoa.

Kingine ni ulaji wa vyakula vya mafuta, kwamba tafiti zinaonesha kuwa vyakula vyenye mafuta kidogo hukosa vichocheo vya ‘progesterone’ ambavyo husaidia kudhibiti nguvu za kiume.

Anasema kuwa progesterone inapopungua huchangia kupoteza nguvu za kiume na matamanio hata kwa upande wa wanawake.

Dk. Mkumbo anasema kuwa nyama na vyakula vyote vya kusindika viwandani huchangia kuangamiza bakteria rafiki (normal flora), ambapo ikitokea hivyo huwa ni chanzo cha magonjwa mbalimbali ikiwamo hili la kupungua kwa nguvu za kiume. “Unapokuwa umeangamiza hawa viumbe katika mfumo wa chakula kwa sababu ya vyakula ambavyo wao hawavitambui, unakuwa ni mtu wa kushambuliwa na maradhi nyemelezi yote hatimaye kudhoofisha ukuta wa mfumo wa chakula.

Baadaye unaweza kuanza kupenyeza sumu (toxins), bakteria wabaya kama E. Coli, vyakula ambavyo havijameng’enywa vizuri na protini zingine kama ‘gluten’ ambazo ni hatari kwa kiafya. “Hivyo, mwanamume anayependelea kula vyakula hivi kwa asilimia kubwa ana uwezekano wa kupungukiwa na nguvu za kiume,” anasema Dk. Mkumbo.

Anawaasa vijana kupendelea kula vyakula asili kwa kuwa husaidia kurudisha uhalisia wa mfumo wa wa chakula kwa kuondoa tatizo la tumbo kujaa gesi na choo kuwa kigumu.

Anataja chanzo kingine kuwa ni sumu zitokanazo na mazingira.

Anasema kuwa watu wengi wanapozungumzia tatizo la nguvu za kiume, wanasahau kulihusisha na mazingira.

Anasema kwa kawaida watu hujishughulisha na kazi mbalimbali ambazo zinawafanya wagusane na sumu; anatoa mfano wa madini ya Zebaki (Mercury) ambayo kwa sasa yapo kila kona.

Anabainisha kuwa madini haya yanaweza kuwa chanzo cha kupunguza nguvu za kiume hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anajenga mazoea ya kuondoa sumu na mionzi mwilini hatimaye kuimarisha afya.

 

MATUMIZI YA DAWA NAYO NI TATIZO

Kwa kawaida tunapokwenda hospitali na kugundulika kuwa tunasumbuliwa na maradhi, tunapewa dawa ili tupone.

Jambo la kushangaza ni kwamba, unaweza kutibu ugonjwa mmoja ukaibuka na mwingine.

Dk. Fredirick Mashili ni daktari bingwa wa fisiolojia ya homoni na mazoezi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili, anasema kuwa kuna baadhi ya dawa zinazotumika kutibu maradhi mbalimbali huchangia tatizo la nguvu za kiume.

Dk. Mashili anasema kuwa licha ya kwamba dawa zote zinazopatikana hospitalini na maduka ya dawa zina lengo la kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali, lakini baadhi yake huambatana na madhara madogo na makubwa kwenye mwili wa binadamu.

Anasema kuwa madhara madogo madogo yanaweza kuwa kichefuchefu, kizunguzungu, kutapika, kuharisha na mengineyo. Wakati madhara makubwa yanaweza kuwa ni saratani, vidonda vya tumbo, ugumba na kuishiwa nguvu za kiume.

 

Dawa za kutibu shinikizo la damu

Dk. Mashili anasema kuwa dawa za kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu hususani zilizo katika kundi ambalo kitaalamu hujulikana kama deutetics (husababisha kukojoa mara kwa mara) pia huchangia kupungua kwa nguvu za kiume.

“Kwa ujumla dawa nyingi zinazotumika kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu, huweza pia kusababisha kupungukiwa kwa nguvu za kiume.

“Kuna dawa nyingi zinazotibu shinikizo la damu ambazo hufanya kazi kwa njia tofauti tofauti – yaani kama ulipewa aina fulani na ikashindwa kufanya kazi, basi unabadilishiwa, lakini nyingine huathiri nguvu za kiume.

Anataja baadhi ya dawa za kutibu shinikizo la damu ambazo huua nguvu za kiume kuwa ni pamoja na Hydrochlorothiazide, Hydropres, Inderide, Moduretic, Oretic, Lotensin, Chlorthalidone (Hygroton), Triamterene (Maxide, Dyazide), Furosemide (Lasix), Bumetanide (Bumex), Guanfacine (Tenex), Methyldopa (Aldomet), Clonidine (Catapres), Verapamil (Calan, Isoptin, Verelan) Nifedipine (Adalat, Procardia) na Hydralazine (Apresoline).

Nyigine ni Captopril (Capoten), Enalapril (Vasotec), Metoprolol (Lopressor), Propranolol (Inderal), Labetalol (Normodyne), Atenolol (Tenormin), Phenoxybenzamine (Dibenzyline) na Spironolactone (Aldactone).

Dawa za kutibu kifafa, msongo wa mawazo na wasiwasi

Anasema kuwa dawa wanazopewa wagonjwa wenye msongo wa mawazo na kifafa, mara nyingi huleta usingizi hivyo kumfanya mtu apate nafuu lakini pia hupunguza nguvu za kiume.

Anatoa mfano wa dawa hizo kuwa ni pamoja na Fluoxetine (Prozac), Tranylcypromine (Parnate), Sertraline (Zoloft) Isocarboxazid (Marplan), Amitriptyline (Elavil), Amoxipine (Asendin), Clomipramine (Anafranil) Desipramine (Norpramin), Nortriptyline (Pamelor), Phenelzine (Nardil), Buspirone (Buspar), Chlordiazepoxide (Librium),Clorazepate (Tranxene),Diazepam (Valium)
Doxepin (Sinequan), Imipramine (Tofranil), Lorazepam (Ativan), Oxazepam (Serax) na Phenytoin (Dilantin).

 

 

Dawa za kutibu mzio (allergy)

Dk. Mashili anasema kuwa dawa hizi mara nyingi hutumika kutibu mafua, miwasho, kutetemeka mwili, kuzuia kutapika na maradhi mengine yanayosababishwa na mzio.

“Licha ya kutibu, dawa hizi pia huchangia kuua nguvu za kiume taratibu.

“Baadhi ya dawa hizo ni Dimehydrinate (Dramamine), Diphenhydramine (Benadryl), Hydroxyzine (Vistaril), Meclizine (Antivert) na Promethazine (Phenergan),” anabainisha Dk. Mashili.

 

Dawa za maumivu

Anasema kuwa dawa ambazo hutumika kutibu maumivu makali ya mwili kama jointi, mgongo na miguu pia huwaathiri wanaume kwa kiasi kikubwa.

Anataja baadhi ya dawa hizo kuwa ni pamoja na Naproxen (Anaprox, Naprelan, Naprosyn) na Indomethacin (Indocin).

“Pia baadhi ya dawa za kupunguza makali ya saratani kama vile busulfan huwafanya wanaume kupungukiwa na nguvu za kufanya tendo la ndoa,” anabainisha.

 

Dawa za kutibu vidonda vya tumbo

Anasema kuwa dawa ambazo hutumika kuponya au kuondoa maumivu makali yanayosababishwa na vidonda vya tumbo, huacha madhara ya aina hiyo.

Dawa hizo ni cimetidine, Nizatidine (Axid) na ranitidine (Zantac).

Dawa za kutibu tezi dume Licha ya kwamba tezi dume hutibiwa moja kwa moja kwa upasuaji, kuna dawa ambazo mgonjwa hupewa kabla ya kufikia hatu ya kupasua.

Dk. Mashili anasema kuwa dawa hizo pia humpunguzia mgonjwa makali ya maumivu.

Anazitaja kuwa ni flutamide (Eulexin) na leuprolide (Lupron), ambazo huwa hazipatikani madukani  bali hutolewa katika hospitali maalumu kama ocean road iliyopo hapa jijini.

 

Dawa za moyo

Mara nyingi dawa za norpace ambazo hupewa watu wenye tatizo la moyo kushindwa kusukuma damu vizuri, huathiri nguvu za kiume.

Dawa nyingine ni zile zinazotumika kudhibiti kusononeka kitaalamu huita ‘depression’ ambazo ni amytriptiline na nyingine nyingi katika kundi hili.

“Dawa zinazotumika kutibu kupaniki na ukosefu wa usingizi kama vile diazepam au valium. “Pia baadhi ya dawa zinazotumika kuzuia milipuko ya kibailojia (anti-inflammatory drugs) kama vile naproxen na indomethacin huwa na tabia ya kuathiri nguvu za kiume,” anasema Dk. Mashili.

Anasema kuwa dawa nyingine ni zile zinazotibu ugonjwa wa Pakinson kama vile Levodopa.

Kwa sababu hii, Dk. Mashili anawashauri watu wenye tatizo la kupungukiwa nguvu za kiume na wanatumia baadhi ya dawa zenye athari kwao, wazungumze na madaktari wanaowatibu ili wabadilishiwe dawa.

Anasema kuwa ni hatari kununua dawa kwenye maduka ya dawa mitaani bila ushauri wa madaktari. Anasema kuwa dawa hizo huleta madhara hayo kwa kuwa huathiri mfumo wa homoni, fahamu au mzunguko wa damu.

“Ni vema mgonjwa kumuuliza daktari wake kuhusu madhara ya pembeni (side effects) ya dawa yoyote anayopewa.

“Kwa mazingira yetu, dawa zenye kuleta tatizo hili zinazotumika sana ni zile za kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba madhara haya huwa ni madogo kuliko madhara yanayoweza kusababishwa na ugonjwa unaotibiwa na dawa husika,” anasema Dk. Mashili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles