21.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

‘Dawa nyingi hazitengenezwi kwa kufikiria kuna Waafrika’

Lagos, Nigeria

WAAFRIKA wenye rangi nyeusi huwa na wakati mgumu wanapohitaji tiba ya dawa kwa sababu wanawakilisha asilimia mbili tu ya sampuli ya vinasaba iliyotumika katika utafiti wa kutengeneza dawa, lakini kampuni mpya ya Nigeria inataka kubadili mfumo huo.

Uhaba wa tafiti kuhusu watu wa aina fulani unahatarisha kuenea kwa magonjwa duniani kote.

Kwa mujibu wa mwasisi na Mkurugenzi wa Kampuni inayoangazia biolojia ya vinasaba ya 54gene, Dk. Abasi EneObong, watu wenye rangi nyeusi wana utofauti wa kimaumbile na watu wengine duniani na kutengeneza taarifa zao za vinasaba kuna uhitaji wa rasilimali kubwa zaidi kupatikana.

Alifanya utafiti wa vinasaba katika maabara ya nchini Nigeria katika mji wa Lagos, timu yake ikiwa na mpango wa kufanyia utafiti vinasaba 4,000 vya sampuli zitakazokusanywa mwaka huu.

Dk. Ene-Obong alisema kuwa ufahamu wa jukumu la vinasaba katika magonjwa litasaidia katika uhusiano wa tiba.

“Dawa hazitengenezwi hata kwa kufikiria kuwa kuna Waafrika wapo, idadi ya Waafrika haifanyiwi majaribio ya kitabibu kulingana na mahitaji yao, kile kilichopo ni dawa ambazo hazina uwezo wa kutibu kiufanisi.

“Dawa mpya pia inachukua muda mrefu kufika Afrika, mara nyingine ni kati ya miaka 15 hadi 20,” alisema Dk. Ene-Obong.

Alisema watengenezaji wakubwa wa dawa huwa wanaangalia soko la mataifa ya magharibi, na aina ya vinasaba vinavyopatikana barani Afrika baada ya kampuni hizo kupoteza wagonjwa wao.

Dk, Ene-Obong alisema anadhamiria kutatua tatizo hili kwa kuongeza upatikanaji wa takwimu za vinasaba kutoka Afrika ili kuhamasisha utafiti wa kisayansi kufanyika zaidi kwa kuwaangazia Waafrika.

“Mpango huo utatoa mwanya wa upatikanaji wa matokeo ambayo yatawafanya Waafrika wapate tiba kulingana nao, lakini pia tiba ya kila mmoja ipatikane,” alisema.

Kampuni yake ina mpango wa kufanyia utafiti magonjwa kama ya selimundu (sickle cell), ugonjwa ambao unawaathiri Waafrika zaidi.

Dk. Ene-Obong alisema 54gene itaweza kubainisha namna ambavyo jenetiki inafanya kazi katika magonjwa ya muda mrefu na yasiyoambukiza kama saratani, shinikizo la damu, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu na mengineyo.

Kwa sasa wameanza katika hospitali za Nigeria ili kukusanya sampuli za DNA.

“Hatutaingilia huduma ambayo wagonjwa wanapata, lakini kwa ruhusa yao tutawaomba kupata damu au tishu za mwilini kwa utafiti,” alisema Dk. Ene-Obong .

Alisema kampuni haina nia ya kuhifadhi tu, lakini pia kuboresha huduma ya afya katika jamii inazozifanyia kazi.

Kampuni hiyo ilipokea ufadhili wa dola milioni 4.5 kutoka kwa wafadhili wakati ilipozindua mradi huo Januari.

Fedha nyingi zilitumika kuongeza maabara zilizopo jijini Lagos, kukodisha wafanyakazi na kutengeneza mfumo wa kusambaza umeme kwa sababu Nigeria inakabiliwa na tatizo kubwa la kukatika umeme.

Dk. Ene-Obong aliacha kazi yake ya ushauri wa viongozi wa sekta ya dawa na kuanzisha kampuni yake ya 54gene, ambayo sasa imeweza kutengeneza watafiti zaidi ya 30 ambao wamefanya kazi katika taasisi za tiba nchini Marekani na Uingereza.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa watu wanatibiwa kwa kiwango kisichokua na utofauti na Marekani au Uingereza,” alisema.

Jina la kampuni hiyo limetokana na majina ya nchi 54 za Afrika.

“Hatutaki kuwa kampuni ya Wanaijeria peke yake, bali tuko na mazungumzo na nchi za Afrika Mashariki, Magharibi na Kusini mwa Afrika,” alisema ingawa alikuwa na hofu kuhusu miongozo iliyopo katika baadhi ya mataifa ya Afrika na kutokuwepo na utayari.

“Tunafuatilia sheria muhimu za kuzifuata katika nchi husika kwa sababu baadhi ya nchi miongozo haiko wazi. Hivyo lazima kujiandaa kufuata sheria husika na kufuata utaratibu wa taifa husika,” alisema Dk. EneObong.

Kampuni hiyo itatunza taarifa ilizozipata kwa kufuata utaratibu.

Kuna baadhi ya Serikali za Afrika kama Kenya na Uganda, mamlaka imependekeza kuwa wakusanye taarifa za vinasaba ambazo zitasaidia kupambana na uhalifu.

Lakini Dk. EneObong alisema kampuni yake haina nia ya kuzigawa taarifa wanazozitafuta ingawa iko radhi kutoa picha kubwa ya takwimu ili Serikali kuweza kuelewa hali ya afya ya watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,717FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles