24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

Dar, Lindi kinara maambukiziya matende,mabusha

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KIWANGO cha maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha katika mikoa ya Dar es Salaam na Lindi, imeelezwa bado kipo juu kwa kati ya asilimia 10 hadi 12.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele, Dk. Upendo Mwingira, alipowasilisha mada katika semina ya kuwajengea waandishi wa habari uelewa wa shughuli wanazozitekeleza na kutoa taarifa ya ugawaji wa dawa kinga kwa wakazi wa Dar es Salaam unaotarajiwa kufanyika Desemba 15 hadi 20, mwaka huu.

Alisema ili kuukabili ugonjwa huo, Serikali ilianzisha mpango huo mwaka 2009 na ziliteuliwa halmashauri 121 zilizoonekana kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi na wananchi kuanza kupewa dawa kinga.

“Tunajua hivi sasa kuna jumla ya halmashauri 185, wakati ule tunaanza mpango tuliteua halmashauri 212 kati ya hizo, 93 sawa na asilimia 77 tumeweza kukabili maambukizi na huko hatugawi tena dawa kinga.

“Zimebaki halmashauri 28 ambazo zina kiwango cha juu, kwa upande wa mikoa ya Dar es Salaam na Lindi ndizo zenye kiwango cha juu zaidi, tunaona Dar es Salaam mwamko wa wananchi kujitokeza kumeza dawa kinga bado ni mdogo.

“Ndiyo maana tunawahamasisha wananchi kujitokeza kumeza dawa kinga hizi, matende na mabusha tunaweza kuyakinga mtu asipate kwa njia hii,” alisema.

Hata hivyo, alisema mtu anapopata busha njia pekee ya kutibu ni upasuaji.

Alisema hadi sasa tayari wanaume 1,000 wamefanyiwa upasuaji wa kutibu mabusha na wapo wengine 3,000 wanasubiri upasuaji huo.

Awali, Ofisa Mpango huo ulio chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Oscar Kaitaba, alisema ugonjwa huo husababishwa na minyoo.

Alisema vimelea vya minyoo hiyo hubebwa na mbu na pindi anapomuuma binadamu huingia ndani ya mwili wake na kwenda kuziba njia ya majimaji.

“Miaka ya zamani ilifahamika kwamba mbu pekee anayeeneza ugonjwa huu ni aina ya culex, lakini tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika duniani zinaonyesha mbu wa aina zote hata yule anayeeneza ugonjwa wa malaria anaweza kueneza ugonjwa huu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,282FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles