29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

DARASSA UNAIKUMBUKA SELFIE YA KOFFIE OLOMIDE?

darassa1

Na CHRISTOPHER MSEKENA

NGOMA inapovuma sana uhai wake huwa mfupi, mbwembwe za mpigaji ni lazima zitaipasua na kufanya wachezaji wasisisikie tena utamu wa ngoma hiyo iliyowapagawisha muda mfupi uliopita.

Napata tabu kuelewa nini kinasababisha nyimbo kali kugawanyika kwenye makundi mawili; kundi la ngoma kali zinazovuma na kupotea baada ya muda mfupi na zile nyimbo kali zinazoishi milele hata zisipopigiwa promo.

Kibongobongo unaweza kusikiliza nyimbo kama Kazi Yake Mola aliyoifanya Mandojo & Domokaya, Kamanda ya Daz Nundaz, Seya wa Papii Kocha & Nguva Viking na nyimbo nyingine zenye haiba ya kutochuja kama hizo.

Kwa kuwa siyo rahisi kupotea kwenye masikio yetu kwa matukio ya misiba na majanga mbalimbali tunajipooza na ngoma kama Kazi Yake Mola au Kamanda na tukiwa kwenye sherehe basi Babu Seya na anatuburudisha kwa ngoma yao ile ya kitambo.

Mawazo yananirudisha nyuma na kuukumbuka mwaka 2015 kuingia 2016. Nyimbo nyingi za Kibongo zilifunikwa, hazikupata nafasi ya kutosha kwenye redio, runinga hata kwenye mitandao ya kijamii sababu Koffi Olomide alisepa na mashabiki.

Toka miaka ya 70 alipoanza kupata nafasi ya kusikika kwenye ulimwengu wa muziki, Koffi tayari ana albamu za kutosha, ameshafanya nyimbo nyingi nzuri zilizomfanya awe miongoni mwa wanamuziki wenye heshima kubwa Afrika.

Oktoba 13, mwaka juzi aliandika historia nyingine ya kulitingisha Bara la Afrika. Koffi alitutia wazimu pale alipoachia Selfie, wimbo uliopambwa na kibwagizo cha Ekotite.

Hii ilileta balaa kwani kizazi hiki ambacho asilimia kubwa kinatumia simu za kisasa kiliucheza wimbo huu, kilivutiwa sana pale anaposema Zua nga Foto ‘Nipige picha mimi’ kisha ala za muziki zilizochanganywa vema zinafuata na kutoa burudani kwa yeyote aliyeusikiliza.

Kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram, video fupifupi zilitawala, mabinti walionyeshana uwezo wa kuzungusha nyonga zao, vijana wa kiume nao kwa mitindo tofauti walionyesha ubabe wa kuucheza wimbo huu.

Nakumbuka mtoto wa H. Baba, Tanzanite alipata heshima ya pekee baada ya video inayomuonyesha akiucheza wimbo huu kumfikia Mopao na akaitupia kwenye ukurasa wake wa Instagram kuonyesha imemgusa.

Nini kilitokea mpaka Selfie ikawa siyo wimbo wenye mvuto tena kwa mashabiki? Mimi sifahamu ila ninachojua Selfie ni wimbo mzuri uliokonga nyoyo za mashabiki na walipouchoka wakaupiga chini ili kupisha nyimbo nyingine.

Novemba 13, mwaka jana Mr. Magic Music, Darassa akaweza kuvunja rekodi ya Selfie kwa mkwaju wake unaoitwa Muziki.

Ni rapa aliyebadilika na kufanya yale ambayo yalidhaniwa hayawezi kufanywa na marapa, Muziki imelata balaa zaidi kuliko Selfie ya Koffi Olomide.

Video yake ndiyo video ya rap iliyotazamwa zaidi mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu. Tukio la hatari kama lile la dereva wa basi kule Dodoma, Said Mkachakacha aliyethubutu kuachia usukani ili tu aserebuke na Muziki wa Darassa, hii ni nadra kutokea.

Utakuwa umeshuhudia video zikiwaonyesha kina bibi, babu, walevi, viongozi wa juu wakionyesha mapenzi yao kwa wimbo wa Darassa.

Ndani ya miezi hii mitatu msanii yoyote alikuwa akitoa wimbo basi hatasikilizwa sababu mashabiki wapo bize na Muziki.

Ninachokiona sasa ni kufanya vizuri kwa zile nyimbo zilizofichwa kipindi kile na nguvu ya Muziki inapungua siku baada ya siku.

Kwa upande wa Koffie nadhani bado anatafuta namna nzuri ya kutoa wimbo utakafanya vizuri kuzidi Selfie hali kadhalika Darassa anaumiza kichwa kipi afanye baada ya Muziki kuonyesha dalili ya kuwa wimbo wa kawaida.

Darassa ana nafasi nzuri, hapaswi kupelekwa na kelele za mashabiki ila anachotakiwa kufanya ni kile kilicho kwenye mipango yake ya kuwafurahisha mamilioni ya mashabiki aliowatengeneza punde alipoachia wimbo wake wa Muziki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles