Na RAYMOND MINJA-MUFINDI
WIMBO wa msanii wa miondoko ya hip pop nchini, Sharif Ramadhan (Darasa), ‘Maisha na muziki’, juzi ulisababisha wanachama wa vyama mbalimbali mkoani Iringa kuondoa tofauti zao kwa muda na kuucheza wimbo huo kwa pamoja.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kwenye kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Walio sahau tofauti za vyama vyao na kuingia kucheza pamoja na wanachama wa CCM ni pamoja na mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia Chama cha Wananchi (CUF) ambaye awali alikuwa amesimama pembeni akifuatilia kilichokuwa kikiendelea katika kampeni hizo.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Katibu wa CCM wilaya hiyo, Jimsoni Muhagamaa, alisema kilichowachanganya wanachama hao wa vyama mbalimbali kujumuika na wana-CCM si muziki huo tu bali wengi wao walikuwa wakifurahia mambo mazuri yanayofanywa na chama hicho kitendo kinachoashiria ushindi tosha katika kata hiyo.
Kampeni hizo zilifunguliwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jeska Msambatavangu.