DARAJA MTO  KILOMBERO KUBORESHA HALI UCHUMI

0
1126
Daraja la Mto wa Kilombero

Na Mwandishi Wetu


WATU wa Mkoa wa Morogoro wanajiweka tayari kwa maendeleo ya uhakika kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero, ambalo lilikuwa kikwazo cha usafiri kwa misimu yote ya masika na  ya kiangazi kwa sababu tofauti na kinzani.

Wakati wa masika maji ya Mto Kilombero huwa mengi na yenye  nguvu kuliko vivuko vinavyowekwa hapo na hivyo kuvisomba na kusababisha ajali mara nyingi na kuua watu wanaovuka.

Wakati wa masika kuna zahama ya kukosekana maji ya kutosha na hivyo vivuko hukwama kwenye mchanga na wakati mwingine katikati ya mto ulionywea na hivyo kufanya wakazi wa Wilaya ya Ulanga na Malinyi kukosa usafiri wa uhakika. Kwa maendeleo yaliyofikiwa, hii sasa ni historia, kwani daraja ni la uhakika.

Mkoa wa Morogoro sasa una wilaya 9 na kuwa mkoa wa kwanza kwa wingi wa wilaya kama Mkoa wa Arusha na hivyo kufikiriwa kugawanywa, kwani ni mkoa pekee wenye wilaya ambazo zina umbali wa kilomita 500 toka makao makuu ya Mkoa. Watu wengi wanafikiria kuwa katika uzinduzi wa daraja itatangazwa taarifa ya kuanzisha mkoa mwingine wa Ulanga. Habari hizo zimezagaa mjini Ifakara.

Daraja la Kilombero lililojengwa na Kampuni ya Wachina limekamilika na hivyo kuwa faraja kwa wakazi wa Wilaya tatu za Kilombero, Malinyi na Ulanga ambao walikuwa wanapata shida ya kuvuka Mto Kilombero kwa vipindi vyote vya mwaka kutokana na mwenendo usiotabirika wa mto huo.

Daraja hilo limeanza kutoa huduma kwa majaribio na huku likisubiri uzinduzi wake na Rais John Magufuli, ambaye akiwa Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano alisimamia na kuhakikisha linajengwa na habari kutoka Ifakara zinasema wakazi wa huko wanasubiri kwa hamu kumuona rais akiwa kama mkombozi wa eneo hilo la wilaya tatu.

Kihistoria baada ya Vita ya Majimaji ambayo ilipiganwa kiume pale Mahenge iliweza kubadili mwelekeo baada ya watu wengi kufa na kudhihirika kuwa dawa ya Kinjekitile Ngwale haikufua dafu kwa bomu bomu za Wajerumani na hivyo Mahenge kufanywa moja ya Wilaya ya mwanzo mwaka 1907.  Muda ulivyoendelea Wilaya iligawanywa na kuwa mbili, ikizaliwa Wilaya ya Kilombero. Halafu mwaka juzi ikaanzishwa Wilaya ya Malinyi kutokana Wilaya ya Ulanga.

Daraja hilo litafungua eneo la kusini na kutoa njia mbadala kwenda Songea kwa kupitia Morogoro, Kilombero, Ifakara hadi Malinyi na Tanganyika kuelekea mkoa wa Ruvuma au Lindi na Mtwara.

Habari zisizothibitishwa na TAMISEMI kwa kukosa msemaji zinasema Tarafa ya Kilolo mkoani Iringa itaunganishwa kwenye Wilaya ya Kilombero na hivyo kuweza kutoa mtandao wa miundombinu mwafaka kwenda na kutoka katika mkoa huo mpya wa Ulanga/Tanganyika  wenye makao makuu yake Ifakara. Ulanga maana yake Bonde la Kilombero ambalo limetapakaa eneo lote na kupakana na Milima ya Udzungwa kwa upande wa Kaskazini Magharibi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesikika kwenye vyombo vya habari kuwa serikali kwa sasa imesimamisha kuunda serikali mpya za utawala hadi itakapomaliza kukamilisha ujenzi wa ofisi, nyumba na kuweka miundombinu stahiki ya mikoa na wilaya zote mpya.

Mazao yanayolimwa kwenye wilaya hizo ni mpunga, pamba, na mazao ya mchanganyiko ya viazi vitamu, ufuta, mihogo, alizeti, ndizi, kahawa miti ya mitiki na miwa. Kuna madini ya Ulanga (mica), kinywe (uno), madini ya vito, ikiwamo ganeti, almasi, dhahabu, yakuti (ruby), mafuta ya petroli na udongo wa mfinyanzi na rare earth elements (REE).

Kutokana na kuweko kwa daraja hilo, usafiri kati ya Dar es Salaam kwenda miji ya Mahenge na Malinyi utapungua muda kwa masaa matatu kutoka saa 12 za sasa hadi saa 9. Utalii upo wa kutosha wa uwindaji katika mbuga ya Selous (Kusini Magharibi), North Frontiers Ulanga, WAMA ya Mofu,  South Ulanga Game na Kibasila Wetlands.

Kwa miaka ya karibuni nchi itegemee mengi kama itaanzizsha mkoa mpya, hasa uchimbaji wa mafuta na uendelezaji wa madini ya kinywe (graphite) huku wananchi wakisubiri kwa hamu mgawo wa umeme wa wa vijijini (REA). Eneo hilo limesahaulika kwa masuala ya umeme wakati ndio chanzo kikuu cha umeme wa maji, ikiwa Kihansi Hydro Power iko Mlimba (MW 170), Chita Tarafa ya Melela lakini utawala wa mradi uko Iringa na hivyo kukwamisha maendeleo ya eneo hilo, kwani asilimia 20 ya mapato kusaidia chanzo yanapelekwa Iringa badala ya Wilaya ya Kilombero; vilevile Kidatu Hydro Power MW 200 nayo iko Kidatu, wilayani Kilombero.

Wadadisi wa mambo wanahoji inakuwaje wilaya hiyo inakosa umeme wa uhakika?

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ulanga (DED), Yusuf Semuguruka, aliviambia vyombo vya habari kuwa uzinduzi wa daraja utafanyika mwezi huu, bila kuainisha tarehe kamili.

Anasema tayari magari ya abiria, yakiwamo mabasi yalikuwa yanatumia daraja hilo na hivyo kupunguza shida za usafiri na kufungua eneo kwa uwekezaji mkubwa na kuendeleza usafiri wa kwenda Mkoa wa Ruvuma na kuachana na matatizo ya kivuko ambacho hakikukidhi mahitaji yanayohitilafiana ya kiangazi na masika.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo, anasema kivuko hicho kitahamishiwa sehemu nyingine ya mto, kwani kuna mahitaji mengi ya vivuko kutoka Wilaya ya Kilombero kwenda Wilaya ya Malinyi na Ulanga ikibeba mizigo na abiria.

Alisema mipango iko mbioni kujenga barabara hadi kiwango cha lami kati ya Lupilo  hadi Malinyi kwenda Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi.

Hata hivyo, maendeleo ya miundombinu hiyo yameleta matatizo kwa wavuvi pale Kivukoni,  Tarafa ya Ifakara, karibu na daraja, kwani pamoja na kuboresha huduma, uchumi wa eneo hilo umeanguka kwa wenyeji, kwani sasa hawauzi samaki wao, kwani magari hayasimami tena na kupita kwa mwendo kasi kwenye daraja hilo.

Hamisi Msati, muuza samaki wa Kivukoni,  analalalamika kukosa soko la samaki zake, kwani wateja hawapatikani kirahisi kufuatia magari kutosimama.

Ujenzi wa daraja utapunguza ajali za kuzama watu wakati wa masika na kwa vivuko kuzama pamoja na kupotea kwa mali zao au kukwama wakati wa kiangazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here