31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

DAR YASIMAMA

*Mvua yaua watu tisa, yakata mawasiliano

*RC Makonda aamuru shule kufungwa, ghorofa lakatika nguzo


Na WAANDISHI WETU-DAR/DODOMA

DAR ES SALAAM imesimama. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo na kusababisha vifo vya watu tisa, huku shughuli za usafiri wa umma zikisimama kutokana na madaraja kufunikwa na maji.

Kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameagiza kufungwa kwa shule zote jijini humo kwa muda wa siku mbili kuanzia leo kama njia ya kuepusha wanafunzi na madhara ya mvua hizo zinazoendelea kunyesha.

Pamoja na hali hiyo imebainika kwamba vifo na majeruhi wa mvua hizo zimetokana na wengi wao kuangukiwa na kuta za nyumba, jambo ambalo limezua taharuki kwa wananchi wa maeneo mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Grace (30) maarufu kama mama Elias na mwanae Abdulrazack ambao ni wakazi wa  Segerea, Mikidadi Hijja(44), mkazi za Salasala, Mwanaidi Seif (42), mkazi wa Kigogo, Amina Said (28), mkazi wa Salasala na mwanafunzi Nasri Hajji ambaye ni mkazi wa Mbagala Mission.

“Watu hao wamefariki baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba ulioathirika na mvua na kupoteza maisha,” alisema Mambosasa.

Kamanda huyo wa Polisi, aliwataja watu wengine waliofariki dunia kutokana na athari hizo za mvua kuwa ni Sadiki Ally (36),  mkazi wa Temeke ambaye aliteleza katika Mto Mzinga na kuanguka. Hadi sasa juhudi za kutafuta mwili wake zinaendelea.

Alisema watu wawili wanaume ambao majina yao bado hayajafahamika, mmoja kutoka Segerea na mwingine Kawe wamefariki dunia baada ya kusombwa na maji, miili ya watu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Kamanda Mambosasa, alisema wananchi wanaoishi mabondeni, nyumba zao zimefunikwa na maji zinaonekana nusu na nyingine hazionekani kabisa.

“Lakini cha kushangaza, wananchi wamedharau hali hiyo na kuendelea na maisha kama kawaida huku wengine wakionekana wamekaa juu ya paa na ukuta bila woga wowote.

“Naomba kuwaambia wananchi wa mabondeni waondoke kwenye maeneo hayo ni hatari kwa maisha, ukuta ukiingia maji tofali zinaloa zinamung’unyuka na nyumba inaanguka na kusababisha maafa, sio mahali salama kwa kuishi, waache ukaidi waondoke,” alisema.

BARABARA ZAFUNIKWA

Alisema lakini pia Jeshi la Polisi limefanya ukaguzi kwa kutumia helikopta na kubaini kuwa katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kijichi, Kigamboni, Jangwani na Buguruni, barabara za maeneo hayo zimefunikwa na maji na nyingine zimekatika kabisa, hivyo basi hazifai kutumika.

Kamanda Mambosasa, alisema katika maeneo hayo wamelazimika kuweka vizuizi maalumu vya kuwaonyesha kuwa, njia hizo zimefungwa kwa muda mpaka maji yatakapokwisha ndipo zitafunguliwa.

“Hivyo basi madereva wanaotumia njia hizo wanapaswa kutii sheria na kufuata maelekezo yaliyotolewa na jeshi ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.

“Jiji la Dar es Salaam limeathiriwa na mvua zinazotoka Wilaya ya Kisarawe na maeneo ya mikoa ya jirani, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa mafuriko, hivyo basi wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari ili kuepusha maafa,” alisema Mambosasa

MAKONDA AAGIZA SHULE KUFUNGWA

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wanafunzi kutokwenda shule kwa siku mbili kuanzia leo hadi mvua hizi zinazoendelea kunyesha zitakapokata.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathirika na mvua katika maeneo mbalimbali ya jiji, Makonda alisema mvua bado zinaendelea kunyesha, hivyo zinaweza kuwaathiri wanafunzi wawapo shuleni.

Alisema kutokana na hali hiyo amezungumza na mamlaka husika akiwamo Ofisa Elimu wa Mkoa (REO) ili waweze kuliangalia suala hilo na kulifanyia kazi.

“Nimezungumza na mamlaka husika ili kuangalia namna ya kuwazuia wanafunzi wasiweze kwenda shule kwa siku mbili hizi ambazo mvua inanyesha, jambo ambalo linaweza kutusaidia kuepusha madhara yatokanayo na mvua kwa wananchi wetu,” alisema Makonda.

Alisema baada ya kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya jiji amebaini kuwa, kuna baadhi ya nyumba zimejengwa kwenye maeneo yanayopitisha maji, jambo ambalo limechangia kujitokeza kwa mafuriko.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi waliojenga na kuziba mitaro ya kupitisha maji, wanapaswa kubomoa nyumba zao ili maji yaweze kufuata mkondo wake.

“Naendelea kuwasisitiza wakazi wa mabondeni, kuondoka kwenye maeneo hayo kwa sababu sio salama, yanaweza kusababisha maafa,” alisema Makonda.

Alisema wananchi wanapaswa kujenga utaratibu wa kuangalia taarifa za habari na kusoma magazeti ili waweze kujua mambo mbalimbali yanayojitokeza, ikiwamo taarifa za kuendelea kwa mvua.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles