32.2 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

Dar yaongoza saratani ya matiti

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaisalage amesema Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa wagonjwa wa saratani ya matiti kutokana na wanawake kukwepa kuzaa watoto wengi na kutokunyonyesha ipasavyo.

Saratani ya matiti kwa sasa inashika nafasi ya pili kwa asilimia 14 baada ya kupanda kutoka nafasi ya nne, huku saratani ya mlango wa kizazi ikishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 56 na Mkoa wa Mbeya unaongoza kwa aina hiyo ya saratani.

Dk. Mwaisalage alisema sababu zingine zinazosababisha ongezeko la saratani ya matiti, hasa kwa maeneo ya mijini ni mtindo na mfumo mbaya wa maisha, uzito kupitiliza, kutokufanya mazoezi na matumizi ya pombe na sigara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam wakati akielezea mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, alisema ni bora sasa wazazi wafikirie kuongeza idadi ya watoto ili wanawake waweze kujitoa katika vihatarishi vya kupata saratani hiyo.

“Saratani zinazoongoza kwanza ni saratani ya mlango wa kizazi, ya pili ni saratani ya matiti, ya tatu ni saratani ya njia ya chakula na ya nne saratani ya ngozi (Kaposi sarcom), ya tano ni saratani inayounganisha sehemu za kichwa na shingoni, ya sita ni saratani ya  tezi, saba ni saratani ya damu, nane saratani ya tezi dume, ya tisa ni satarani ya kibofu cha mkojo na ya kumi ni saratani ya ngozi inayowaathiri albino.

“Saratani ya matiti inaendelea kuongezeka kwa kasi, tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, tunahamasisha unyonyeshaji ili kupunguza vichocheo vinavyoenda kuathiri matiti.

“Suala jingine ni kuwa na watoto wa kutosha. Huku mjini mtu anakuwa na mtoto mmoja au wawili,  lakini ukiwa na watoto kuanzia wanne, uwezekano wa kupata saratani ya matiti unapungua. Pia tunaendelea hata kuhamasisha upimaji kwa wanawake na watoto,” alieleza Dk. Mwaisalage.

Akielezea namna uzazi unavyosaidia kuepukana na saratani ya matiti, daktari bingwa wa saratani, Crispin Kahesa alisema mwanamke anapozaa, homoni za uzazi za oestregen zinakuwa katika uwiano unaolingana ambapo hali hii huepusha saratani.

“Mwanamke kuzaa kunaendana na mzunguko wake wa hedhi, hivyo vyote vinasababishwa na homoni, mama anapozaa homoni ‘zina-balance’ (zinaweka usawa) na mama ambaye hazai kuna baadhi ya homoni ‘hazi-balance’, hasa homoni zinazohusishwa na saratani ya matiti za oestrogen. Hizi lazima ziwe na uwiano mzuri, kuzaa kunasaidia homoni ziweze ‘ku-balance’ vichocheo vya mwili vizuri.

“Vichocheo hivyo havitakiwi kukatizwa, vikikatizwa vinaleta mabadiliko yasiyo sahihi kwenye chembechembe za matiti, kwa hiyo vinaweza  kuongeza hatari ya saratani ya matiti. Hivyo kuzaa na kuonyonyesha kunasaidia ku-balance vichocheo,” alisema Dk. Kahesa.

Alisema suala la ulaji wa vyakula, hasa vinavyokaushwa, vina uwezo wa kusababisha saratani ya ini kutokana na vyakula hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha sumu aina ya kuvu.

 “Kuna saratani inatokana na uhifadhi wa chakula au kinavyokaushwa, iwe mahindi, mihogo, uwele ambao haujahifadhiwa vizuri, hivi vinaweza kutengeneza sumu  kuvu, ambavyo vinaweza kusababisha saratani ya ini, hizi zinatokea sana ukanda wa kati,” alisema Dk. Kahesa.

MAFANIKIO YALIYOPATIKANA

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, alisema Serikali ilinunua mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi aina ya LINA na CT Simulator ili kuimarisha huduma za tiba ya saratani.

“Kabla ya kununua mashine hizo, kulifanyika ujenzi  wa jengo ambao uligharimu Sh bilioni 2.3 na ununuzi wa mashine hizo uligharimu  Sh bilioni 9.5. Kutokana na mashine hizo jumla ya wagonjwa 1,141 walitibiwa, takribani wagonjwa 208 wangepelekwa nje mashine hizi zisingekuwepo,” alisema Dk. Mwaisalage.

Alisema uwepo wa mashine hizo umeokoa kiasi cha Sh bilioni 10.4 ambazo zingetumika kutibu wagonjwa nje ya nchi.

Dk. Mwaisalage alieleza kuwa mafanikio mengine ni uwepo wa dawa za saratani kwa asilimia 95 ambapo bajeti ya ununuzi wa dawa iliongezwa kutoka milioni 77 hadi bilioni 7 kwa kila mwaka.

Aidha alibainisha kuwa Serikali inaanza kutekeleza miradi mipya katika taasisi kwa kutoa Sh bilioni 14.5 kwa ujenzi wa jengo maalumu (Bunkers) na kununua na kusimika mashine mpya za kisasa za Cyclotron na PET/CT Scan.

“Upatikanaji wa vipimo hivi nchini utapunguza gharama zitokanazo na kupeleka wagonjwa nje ya nchi, hivyo Serikali itaokoa Sh bilioni tano kwa mwaka. Mradi huu pia utahusisha kujenga kiwanda (cyclotron) cha kutengeneza dawa za nyuklia (radio-isotopes) ambazo zitatumika kuweka wagonjwa kwenye upimaji wa PET/Scan,” alisema Dk. Mwaisalage.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles