26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 17, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dar yajipanga kukusanya Sh bilioni 140 mwaka 2025/2026

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejiwekea lengo la kukusanya na kutumia Sh bilioni 140 katika mwaka wa fedha wa 2025/2026 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10 kulinganisha na bajeti ya sasa.

Hayo yamesemwa Februari 11,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Wilaya ya Ilala kilichokuwa na lengo la kupitia bajeti ya 2025/2026.

Amesema asilimia 70 ya bajeti hiyo itakwenda kuhudumia wananchi katika miundombinu ya afya, elimu na barabara pamoja na kuwawezesha kiuchumi kwenye makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Aidha amesema wataangalia fursa zinazopatikana katika jiji hilo kwa lengo la kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati.

“Jiji la Dar es Salaam linakwenda kujitegemea, kipindi hiki ambacho baadhi ya mataifa yanaanza kujitoa kufadhili sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunajitegemea katika utekelezaji wa miradi, eneo la afya, sekta ya elimu na nyingine, bajeti hii inajikita katika kujitegemea na siyo kuwa tegemezi,” amesema Mabelya.

Amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 walijiwekea lengo la kukusanya Sh bilioni 130 na katika kipindi cha miezi sita kufikia Desemba 2024 imekusanya zaidi ya Sh bilioni 79 sawa na asilimia 62 ya bajeti.

“Tunaamini mpaka robo ya sasa itakapoisha tutakuwa tumekaribia lengo la bajeti kuu la kukusanya Shilingi bilioni 130, tunayo matumaini makubwa kwamba tutakusanya zaidi ya bajeti ambayo tumeipanga kutokana na juhudi ambazo tunaendelea kuzifanya.

“Tumeziba mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha mifumo yetu ya kifedha na ukusanyaji mapato tunaiimarisha na kuiboresha, tunaendelea kutoa elimu kwa walipakodi katika kata zetu zote 36 na kanda saba zimetusaidia kwa sababu matokeo tunayaona ya ufanisi na utoaji huduma kwa wananchi,” amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameipongeza halmashauri hiyo kwa mwenendo mzuri wa ukusanyaji mapato na kuishauri kutenga bajeti ya kutosha kwenye eneo la mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Mheshimiwa rais amekuwa ‘champion’ wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, umefanyika mkutano mkubwa unaohusu masuala ya nishati yote haya yanaonyesha namna Serikali ilivyojipanga katika eneo hili ndiyo maana tumeshauri Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na kaulimbiu ya Serikali kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

“Tumeshauri watenge bajeti ya kutosha kwenye eneo la mazingira kwa sababu tumekuwa tukipokea wageni wengi katika jiji letu kwahiyo mazingira yanatakiwa kuendelea kuboreshwa, kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katikati ya jiji ni eneo ambalo linatakiwa kuendelea kuboreshwa,” amesema Mpogolo.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema pia maandalizi ya Soko la Kariakoo kufanya biashara kwa saa 24 yanaendelea vizuri na wafanyabiashara wamepokea vizuri uamuzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
595,000SubscribersSubscribe

Latest Articles