Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Katika kuhakikisha wanafunzi wa sekondari hawapati daraja nne na sifuri Mkoa wa Dar es Salaam umeweka mkakati wa kuhakikisha wote wanafaulu.
Uamuzi huo umekuja baada ya kuongezeka kwa kiwango cha wanafunzi wanaopata daraja la nne na sifuri kwa miaka mitatu mfululizo katika baadhi ya shule za Manispaa ya Temeke zikiwemo za Pendamoyo, Diplomasia na Ndalala.
Katika Shule ya Sekondari Diplomasia matokeo yanaonyesha kati ya mwaka 2022 hadi 2024 wanafunzi 596 walipata daraja la nne na 321 walipata sifuri.

Aidha katika Shule ya Sekondari Pendamoyo matokeo yanaonyesha kati ya mwaka 2022 hadi 2024 wanafunzi 342 walipata daraja la nne na 350 walipata sifuri.
Vilevile kwa Shule ya Sekondari Ndalala matokeo yanaonyesha kati ya mwaka 2022 hadi 2024 wanafunzi 564 walipata daraja la nne na 322 walipata sifuri.

Akizungumza leo Februari 10,2025 wakati wa mkutano na wakuu wa shule za sekondari zilizopo Manispaa ya Temeke, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na matokeo mazuri na kuwa na mchango mzuri katika taifa.
“Tutafanya tafiti za kina kubaini sababu zinazochangia kuwa na matokeo mabaya, tutakaa na wenyeviti wa bodi za shule za msingi na sekondari, walimu pamoja na wazazi na kujadiliana kuhusu changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Chalamila.
Naye Ofisa Elimu Taaluma Manispaa ya Temeke, Mwanaidi Torroha, amesema changamoto kubwa ambayo imechangia kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika shule hizo ni utoro, uhaba wa walimu, ushirikiano duni wa wazazi, wanafunzi kutoelewa lugha ya kingereza na wanafunzi wengi wanaowapokea kuwa na ufaulu wa daraja C.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema ili kukabili changamoto ya upungufu wa walimu wanatarajia kuajiri walimu wapya 200 wa masomo ya sayansi na hesabu, kujenga shule mbili mpya za sekondari na kuendelea kukamilisha shule za sekondari za ghorofa zilizoanza kujengwa mwaka jana.