29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Dar kuwasaka ambao hawajaanza matibabu ya kifua kikuu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka mikakati kabambe ya kuwatafuta wagonjwa wa kifua kikuu ambao hawajabainika ili waanzishiwe matibabu kuepuka kuambukiza watu wengine katika jamii.

Kwa mwaka 2021 ilikadiriwa watu 133,000 waliugua kifua kikuu nchini lakini waliogundulika na kuanzishiwa matibabu ni 87,119 huku Mkoa wa Dar es Salaam ukichukua asilimia 22 ya wagonjwa wote nchini.

Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa kwenye mafunzo kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu yaliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Aidha takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO 2021) zinaonyesha Tanzania ni kati ya nchi 30 duniani zenye wagonjwa wengi ambapo huchangia asilimia 87 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu.

Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Seif Mbarouk, amesema mgonjwa ambaye hajaanza tiba ana uwezo wa kuambukiza watu 15 hadi 20 kwa mwaka.

Dk. Seif alikuwa akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na halmashauri hiyo kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani inayoadhimishwa Machi 24 kila mwaka.

“Ni jukumu letu kuendelea kuwatafuta na kuwaweka kwenye matibabu ili kupunguza maambukizi ya kifua kikuu katika jamii zetu na kutokomeza ugonjwa huu nchini,” amesema Dk. Mbarouk.

Naye Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Wilaya ya Kifua Kikuu ya Mnazi Mmoja, Dk. Linda Mutasa, ameiasa jamii kutowanyanyapaa wagonjwa wa kifua kikuu kwani wakishameza dawa kwa wiki mbilli uwezo wa kuambukiza hupungua kwa zaidi ya asilimia 80.

Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Wilaya ya Kifua Kikuu ya Mnazi Mmoja, Dk. Linda Mutasa, akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu.

Aidha amesema kupitia elimu itakayotolewa na vyombo vya habari wanatarajia itaongeza ufahamu katika jamii kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu, kupunguza au kuondoa unyanyapaa na kuongeza ushiriki wa wadau katika udhibiti wa ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Elizabeth Nyema, amesema vyombo vya habari vina uhumimu katika mapambano ya ugonjwa huo kwani vinasaidia kufikisha elimu kwa wananchi waweze kujua dalili mapema, kufika kwenye vituo vya afya na kujikinga na kukinga wenzao.

“Tuna changamoto kubwa upande wa kuwaibua wateja, pia tuna changamoto kwa elimu kuifikia jamii na aina ya watu wanaowaficha wagonjwa wa kifua kikuu, tunaamini wanahabari wakielewa na kutoa ujumbe ulio sahihi kwa pamoja tutamaliza kifua kikuu,” amesema Dk. Nyema.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema ‘Okoa maisha wekeza katika kutokomeza kifua kikuu nchini’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles