MIUNDOMBINU DAR KUFUMULIWA UPYA

0
1172

NA EVANS MAGEGE – dar es salaam

MRADI wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka zenye urefu wa kilometa 138.6 ambazo zimegawanywa katika awamu sita na barabara za juu (Flying over) tano, ni dhahiri utafumua upya miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam na kuwa kwenye mwonekano mpya.

Hatua hiyo inatokana na jiji hilo kukabiliwa na msongamano wa magari ambao kila siku husababisha hasara ya Sh bilioni 4.

Tayari awamu ya kwanza imekamilika ambayo imehusisha barabara yenye urefu wa kilometa 20.9, huku ujenzi wake ulifadhiliwa na Benki ya Dunia (WB). Utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 na kukamilika Desemba mwaka jana.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema gharama za awamu ya kwanza ya ujenzi huo, zilifikia Sh bilioni 403, kati yake Sh bilioni 317 zilitolewa na Benki ya Dunia huku Serikali ikitoa Sh bilioni 63 kwa ujenzi huo. Sh bilioni 23.5 zililipwa kama fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo.

Baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, awamu ya pili inatarajiwa kuwa ujenzi wa barabara ya kilometa 19.3 kutoka Gerezani Kariakoo hadi Mbagala Rangi Tatu.

“Ndani ya mradi huu namba mbili kuna barabara nyingine ya Chang’ombe hadi Jitegemee na kutakuwa na fly over kwenye makutano ya barabara ya Chang’ombe na Uhasibu,” alisema.

Awamu ya tatu itakuwa ni barabara yenye urefu wa kilometa 23 itakayounganisha barabara ya Mtaa wa Uhuru, Bibi Titi Mohamed hadi Gongo la mboto.

Alisema awamu ya nne itakuwa ni barabara yenye urefu wa kilometa 25, itakayoanzia barabara ya Bibi Titi, Ali Hassani Mwinyi kuelekea Bagamoyo.

Awamu ya tano itajumuisha barabara yenye utefu wa kilometa 22.8 ambayo itahusisha Barabara ya Mandela, huku awamu ya mwisho itakuwa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 27.6 kwa barabara ya Mwai Kibaki.

Mbali na barabara za mwendokasi, pia kuna ujenzi wa barabara za juu.

Mbali ya barabara za juu za Ubungo Mataa ambayo inatarajiwa kufadhiliwa na Benki ya Dunia na ile ya Tazara ambayo ujenzi wake umeanza, nyingine ni zitakazojengwa kwenye makutano ya barabara za Nyerere na Kawawa eneo la Chang’ombe Veta, Kilwa na Mandela.

 

RAIS MAGUFULI

Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo uliofandhiliwa na Benki ya Dunia, Rais Dk. John Magufuli alisema awamu ya pili itafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Alisema awamu ya tatu na nne na tano zitafadhiliwa pia na Benki ya Dunia, huku benki hiyo pia ikifadhili usanifu wake.

Rais Magufuli alisema Dar es Salaam ni jiji kuu la biashara nchini na pia ni miongoni ya majiji yanayokua kwa kasi barani Afrika.

“Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 5 na unaposema milioni tano Tanzania nzima tupo milioni 50, kwa hiyo ukigawa kwa hesabu za haraka unapata moja ya kumi ya Watanzania ni wakazi wa Dar es Salaam… kwa hesabu za Kizaramo za harakaharaka inamaanisha kila palipo na watu 10 mmoja anaishi Dar es Salaam.

“Ndugu zangu adha za msongamano wa magari barabarani sote tunazifahamu, kwanza ongezeko la ajali, watu wameshindwa kufika makazini kwa wakati na inawezekana kuna ndoa zimevunjika kwa sababu ya kuchelewa kufika nyumbani, huduma za uokoaji nazo zimekuwa tatizo, lakini upotevu wa fedha pia umekuwapo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema inakadiriwa kwamba kabla ya mradi wa mabasi yaendayo haraka haujaanza, wananchi walikuwa wanatumia saa mbili hadi tatu kutoka Kivukoni hadi Kimara, lakini kwa sasa wanatumia dakika 30.

Rais alisema utafiti uliofanyika mwaka 2013, nchi ilikuwa inapoteza Sh bilioni 411.55 kwa mwaka kutokana na tatizo la msongamano wa magari barabarani.

Aliongeza kwamba katika jitihada za kutatua changamoto ya msongamano wa magari, Serikali ilibuni mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa mpango wake mkubwa katika kufanikisha awamu ya kwanza ya mradi huo.

Pia aliwashukuru Benki ya Dunia kwa mshikamano na ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mradi huo.

“Lakini namshukuru sana mkandarasi kwa kazi kubwa, nakumbuka wakati anajenga, pale Manzese watu walipanga nguo ndani ya barabara. Inawezekana watu mmeishasahau, lakini alisimama mpaka akamaliza kazi.

“Lakini kama mnakumbuka tena kuna watu walimvunja moyo kwa sababu tatizo la Watanzania kila mmoja ni mkandarasi, barabara zilipokuwa zikitengenezwa wengine walisema barabara ni nyembamba mno kwamba magari makubwa hayataweza kupita, lakini nina uhakika sasa wanayaona yanapita,” alisema Dk. Magufuli.

Kutokana na hali hiyo aliiomba Benki ya Dunia kuharakisha mchakato wa kutoa fedha ili barabara za juu eneo la Ubungo Mataa zijengwe kuwezesha mabasi ya mwendokasi kufanya kazi bila kikwazo cha foleni kilichopo sasa hivi.

“Hauwezi kuwa mradi wa kwenda haraka kwa sababu itabidi tuweke askari wa usalama barabarani na aamue yeye kuruhusu magari kwa kadiri ya uharaka wake, upolepole wake anavyotaka. Kwa hiyo naomba sana kwa Makamu Rais wa Benki ya Dunia kwa upande wa Afrika, kwamba ujenzi wa Ubungo ‘interchange’ ni muhimu sana.

“Upembuzi yakinifu wa interchange ile umeishafanyika  na mkandarasi yupo kwenye mchakato wa kupatikana, interchange ile ikijengwa itakuwa na ghorofa tatu na hatahitajika tena askari wa usalama barabarani kusimama pale,” alisema.

Rais Magufuli alisema kuwa mbali na barabara hizo za mabasi yaendayo haraka, Serikali imejipanga kujenga miundombinu mingine ya mawasiliano ya barabara kwenye maeneo ya Mwenge, Morocco, Magomeni, Tabata na Tazara.

Aliongeza kuwa Serikali imetenga Sh bilioni 38 kwa ujenzi wa barabara za Jiji la Dar es Salaam na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutalifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kwenye sura mpya.

 

TRENI YA UMEME

Rais Magufuli alisema: “Pia hivi karibuni tunapitia tenda ya kupata kandarasi wa kuweza kujenga treni ya kutumia mafuta na umeme ambayo itatoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo urefu ni kilometa 200. Na treni hii itakuwa ya kutoka Morogoro kwenda Dodoma na tutaendelea hivyo tutafika hadi Mwanza na tutafika hadi Rwanda na Burundi.

“Lakini pia mchakato wa kupata barabara za haraka kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze unaendelea, ile barabara itakuwa na njia sita na hatua zote zimeishakamilika, imebaki sasa makandarasi waendelee katika mazungumzo ya kuhakikisha kwamba tunajenga.

“Tunataka kumwomba Rais wa Benki ya Dunia watufadhili katika ujenzi wa treni nyingine ya kutoka bandarini kwenda Ruvu ili magari yanayotoka mikoani yasiwe yanalazimika kuja Dar es Salaam, ambayo nayo yanasababisha msongamano. Kwa hiyo kwa pale Ruvu tutajenga bandari ya nchi kavu (ICD) ili magari makubwa yawe yanachukulia mizigo huko,” alisema.

 

ATAKA KUJUA FAIDA KWA DART

Akizungumzia taarifa zilizotolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, George Simbachawene, Prof. Mbarawa na viongozi wa DARTS, Rais Magufuli alisema kuwa alikuwa anasubiri apewe taarifa ya mapato.

“Nilikuwa nasubiri wanipe taarifa kwamba tangu mradi huu uanze wameishatengeneza hela kiasi gani? Lakini wamekwepa wee sasa sifahamu kama ni makusudi au mradi huu tumeuanza unapata hasara au umepata faida, lakini nimewaachia hii changamoto kwao.

“Nataka leo jioni mawaziri hawa wawili na wasimamizi wa DARTS waniambie walikuwa wanatengeneza faida kiasi gani na kama majibu wanayo, nikimaliza hotuba yangu waje hapa watoe taarifa.

“Watanzania wanataka kujua faida ya mkopo waliokopa kama ni hasara au bomu, wajue mkopo huu kama fedha zinakwenda mifukoni mwa watu au la kwa sababu nataka nijue kama fedha hizo za faida zipo tuzipeleke kwenye miradi mingine,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here