Na Mwandishi Wetu, Mtanzaia Digital
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, amesema wanajivunia kwa kampeni ya Safisha Pendezesha Dar es Salaam na sasa wako tayari kupokea wageni wanaotaka kuja kuwekeza na kutalii kwa kuwa jiji hilo ni safi.
Akizungumza jana Aprili 30,2022 wakati wa usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi uliofanyika katika baadhi ya maeneo ya Kata ya Buguruni, Makala amesema kampeni hiyo ni endelevu kwa kuwa jiji hilo ni mojawapo ya lango la wageni wanaoingia kutoka nje.
Amesema kampeni hiyo imesaidia kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji la mfano na kuliwezesha kushika nafasi ya sita Afrika katika usafi wa mazingira.
“Hatuwezi kujikubali lakini utafiti uliofanyika katika Afrika Dar es Salaam ni jiji la sita Afrika kwa usafi. Kampeni yetu imefanikiwa baada ya kudhibiti biashara holela na kuwapanga vizuri wamachinga tunataka kuona wakati wote mitaa yetu inakuwa safi…usafi unaanza na wewe nyumbani.
“Kazi aliyoifanya mheshimiwa Rais ya kuitangaza Tanzania Dar es Salaam hatuna aibu tena ya kupokea wageni,” amesema Makala.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amesema baada ya kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo baadhi yao wameendelea kurudi katika maeneo yasiyoruhusiwa na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Aidha katika zoezi hilo pia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amemkabidhi mkuu huyo wa mkoa mapipa 20 ya kuhifadhia taka na mafagio yaliyotolewa na wadau mbalimbali.