Dar, Shaanxi kushirikiana kibiashara

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesaini makubaliano ya awali ya ushirikiano kati na Jimbo la Shaanxi-China katika nyanja mbalimbali

Akizungumza jana Novemba 27, 2023, Chalamila amesema tayari wamesaini hatua za awali kuonesha makubaliano ya kuanza mchakato wa mashirikiano.

Amesema baada ya makubaliano kinachofuata ni nyaraka ya kisheri iliyopitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kisha hatua nyingine.

“Kwa nini tumefikia makubaliano haya kwa sababu Dar es Salaam ni jiji ambalo linakua na ifikapo mwako 2030 ni jiji la saba katika Afrika na lango la kibiashara,”amesema Chalamila.

Chalamila amesema wamepokea wageni 30 kutoka jimbo la Shaanxi wote wamekuja kwa ajili ya utekelezaji na wapo tayari kushirikiana, kuhakikisha wanakuwa pamoja ma sekta binafsi, Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kushirikiana zaidi kubadilisha ujuzi na uzoefu hivyo Dar es Salaam kutakuwa na wimbi kubwa la viwanda na wafanyabiashara wakubwa kutoka China.

“Tunategemea fursa nyingi za uchumi zitafunguka tunatii agizo la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kukua kwa miji nchini, “amesema.

Pia amesema EMU ambayo inakubaliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaeleza maeneo yote ya mashirikiano ikiwemo elimu, afya, viwanda, biashara, miundombinu, kilimo, madini na utalii.

Naye Balozi wa China nchini ,Chen Mingjian amesema Jimbo la Shaanxi nchini China ni miongoni mwa majimbo yenye mapinduzi ya teknolojia katika sekta ya elimu na viwanda, hivyo kuanzisha ushirikiano na Mji wa Dar es Salaam ni fursa nzuri kwa sababu ni mji ambao pia ni kitovu cha usafiri ukihudumia nchi nane jirani zisizo na bandari.

Amesema China na Tanzania zimekuwa marafiki wa muda mrefu na wameingia mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya mataifa hayo ambayo yamechagiza kuboresha biashara na maendeleo ya watu.